Katika mahojiano maalumu na taasisi hiyo kuhusiana na suala la
kukatwa watu miguu, imeelezwa kuwa ukataji huo wa viungo ni sehemu ya
tiba ya katika kuokoa maisha.
Pamoja na kutoa maelezo hayo ya sababu za kukatwa kwa viungo pia
taasisi hiyo imesema kwa muda wa mwaka sasa inakabiliwa na changamoto ya
kupata viungo bandia vikiwemo miguu na mikono kwa ajili ya kuwawekea
watu waliopata ajali mbalimbali, magonjwa ya kansa na kisukari ambayo
yamesababisha watu kupoteza viungo vyao.
Changamoto hiyo inatokana na ukweli halisi kuwa kwa siku za hivi
karibuni kila siku mtu mmoja, wawili na wakati mwingine watatu hufika
katika taasisi hiyo kwa ajili ya kuhitaji viungo bandia.
Sababu ya kiungo kukatwa Mkurugenzi wa Tiba MOI, Dk. Samuel Swai
katika mahojiano maalum na gazeti hili jana alisema kama viungo vinakuwa
vimeharibika sana husababisha hatari katika maisha ya mhusika na hivyo
ni muhimu kukiondoa.
Alisema hayo wakati akifafanua taarifa yake kwamba katika idadi yote
ya majeruhi wanaowapokea, kila watu 50 wanaofika kunakuwepo na moja
ambaye anakuwa ameumia zaidi mguu ama mkono ambao mwishowe inabidi
uondolewe.
“Katika kiungo hicho kinachokuwa kimeumia sana ambacho hakiwezi
kubaki, unakuta mishipa ya damu na fahamu imeharibika. Hata kama mguu
ama mkono huo utapona hautaweza kutembea. Inatokea na kulazimu kukata
viungo hivyo.“
Madai ya bodaboda kukatwa makusudi Alitoa angalizo kuwa kuna dhana
potofu iliyojengeka katika jamii kuhusu taasisi hiyo kuwa, wale
walioumia na pikipiki wanapofika katika taasisi hiyo wanakatwa mguu
hivyo alikanusha hilo na kusema si kweli kwani uamuzi wa kumkata mguu
ama mkono mtu yeyote unafanywa na jopo la madaktari wanaokaa na kuona
kiungo hicho hakiwezi kutumika tena.
“Tunashauriana na wataalamu wa mishipa ya damu na fahamu kuhusu mguu
ama mkono huo, endapo unakuwa umeharibika sana. Hatukati kiungo hicho
ovyo ovyo ni lazima mgonjwa ama ndugu aridhie.
“Baada ya kukatwa mguu au mkono, mgonjwa akishapona tunaangalia uwezo
wa kutembea au kutumia mkono unafanya kazi namna gani.
Kwa kukata mguu
kuna uwezekano kabisa ya kumtengenezea mguu wa bandia kiasi akawa
anatembea na kuendesha gari. Mguu huo unaweza kuwa mfupi chini ya goti
au mrefu juu ya goti,” alisema Dk Swai.
Miguu bandia ya kukimbia Mtaalamu huyo alisema ni maono yao kama
taasisi kwa siku za baadaye kuweza kutengeneza mguu au miguu
itakayomwezesha mtu anayehitaji kuweza kukimbia.
“Ni miguu miepesi, inatengenezwa kitaalam kabisa hapa kwetu
hatujafikia utaalamu huo,” alisema. Alieleza changamoto kubwa
wanayokutana nayo ni kuagizwa kwa vifaa hivyo nje ya nchi ambavyo ni
ghali.
Kwa maelezo ya Dk Swai, miguu mizuri inayoagizwa nje gharama yake inakuwa kubwa kiasi kwamba mtu wa kawaida hawezi kuimudu.
Gharama ya mguu bandia chini ya goti ni Sh 600,000 na juu ya goti ni Sh milioni 1.5.
Kwa upande wa mikono juu ya kiwiko ni Sh. milioni 2.5 na chini ya
kiwiko ni Sh milioni 1.5. Akizungumzia utengenezaji wa viungo hivyo
bandia iwe ni mguu au mkono alisema kuwa vinachukua muda wa kama mwezi
mzima hadi miezi miwili kwani mchakato wake ni mrefu.
Alisema kama taasisi wamejitahidi kuzungumza na Mifuko ya Bima ili waweze kuweka gharama hizo za viungo kwa kuwa zipo juu.
Akizungumzia majeruhi anayetaka kuvaa kiungo bandia alisema
inategemeana na alivyoumia kwani hupona ndani ya miezi mitatu hadi sita.
Akizungumzia suala la ukataji wa viungo katika taasisi hiyo, alisema
ndani ya miezi mitatu anakuwepo mtu wa kukatwa kiungo, lakini mara
nyingine kwa mwezi moja hukatwa wawili au watatu inategemeana. Kushamiri
kwa imani za kishirikina.
Ametoa angalizo kuwa kutokana na mila za kiafrika watu wengi wanakuwa
na uoga mkubwa wa kukata kiungo chochote, na kwamba imeshafikia wakati
mgonjwa anakaribia kufa kutokana na sumu anayopata kutokana na
kuharibika kwa kiungo, ndugu wanakuwa wanakataa kabisa asikatwe.
“Ndugu wengine wanasema kuliko mgonjwa akatwe kiungo chake ni bora
waondoke naye,” alisema na kuongeza kuwa katika hilo elimu inahitajika
jamii kulikubali suala hilo.
Alisema kauli mbiu yao ni kuhakikisha wanaponyesha maisha ya mgonjwa
na kuokoa kiungo cha binadamu kisikatwe, na kiokolewe kiungo ambacho
kikibakizwa kinaweza kufanya kazi, hivyo hatua ya kukata kiungo inakuja
mwisho baada ya jitihada zote kushindikana.
Alisema kwa watoto wanaowekewa viungo kwa kuwa wanaendelea kukua
inabidi kila baada ya miezi sita kurudi hospitali na kutengenezewa tena.
Mtaalamu wa viungo bandia katika taasisi hiyo, Charles Mahua alisema
kwa mwaka wanapokea zaidi ya watu 100 wanaohitaji viungo bandia, kwani
kila siku amekuwa akishuhudia mtu mmoja hadi watatu wanafika kwa ajili
ya huduma hiyo.
“Hivi sasa kuna kesi za ajali za barabarani, ugonjwa wa kisukari na
kansa ambazo zote hizo zinasababisha watu kupoteza viungo,” alisema
Mahua.
Alisisitiza kuwa ukosefu wa vifaa endelevu ndio changamoto kubwa
katika taasisi hiyo kwa kuwa wanaweza kupata vifaa halafu vinaisha.
Alisema zaidi ya mwaka walikuwa hawana vifaa, lakini miezi miwili
iliyopita walipata miguu 400 bado wanahitaji mikono. Alisema wananchi
wengi hawana uwezo wa kulipia gharama halisi, na kwamba kwa sasa bima ya
afya huwa hailipi katika eneo hilo.
Alisema changamoyo nyingine ni upungufu wa wafanyakazi kwani kama
wangekuwa na vifaa vyote, watumishi wa afya wa kutoa huduma pia
wasingetosha.
chanzo;habarileo.
Comments