Wasichana wang'ara kidato cha pili.

BARAZA la Mitihani Tanzania (Necta) limetangaza matokeo ya upimaji wa kitaifa wa kidato cha pili ambapo ufaulu umeongezeka kwa asilimia 1.9 huku wasichana waking’ara. Pia limetangaza matokeo hayo kwa darasa la nne.
Aidha, wanafunzi wa kike wameng’ara katika mitihani hiyo huku Mkoa wa Mtwara umeonekana kufanya vibaya kwa kuwa na shule tisa kati ya 10 zilizofanya vibaya.
Akitangaza matokeo ya kidato cha pili, Katibu Mtendaji, DK Charles Msonde alisema jumla ya wanafunzi 372,228 ambao ni asilimia 91.02 wamepata ujuzi na maarifa ya kuwawezesha kuendelea na kidato cha tatu.
Alisema ufaulu huo umeongezeka kwa asilimia 1.9 ukilinganisha na ufaulu wa mwaka 2015 ambapo wanafunzi 324,068 ambao ni asilimia 89.12 waliopata alama za kuwawezesha kuendelea na masomo ya kidato cha tatu.
Msonde alisema idadi ya watahiniwa waliopata ufaulu mzuri wa daraja la I, II na III ni wanafunzi 178,115 sawa na asilimia 43.55, wasichana wakiwa ni 78,466 sawa na asilimia 37.45 na wavulana 99,649 ambao ni asilimia 49.97.
Akizungumzia ufaulu wa masomo, Msonde alisema ufaulu wa masomo ya Civics, History, Geography, Kiswahili, Fizikia, Kemia, Bayoloji na Hisabati umepanda ukilinganisha na mwaka 2015. Ufaulu wa somo la Kiingereza pekee ndio ambao umeshuka ukilinganisha na mwaka 2015.
“Somo lililofanya vizuri zaidi ni Kiswahili ambalo asilimia 90.06 ya wanafunzi wamefaulu huku Hisabati ikiwa na ufaulu wa chini ambalo waliofaulu no asilimia 21.55,” alisema.
Aidha Msonde alizitaja shule zilizofanya vizuri kuwa ni, St Francis Girls(Mbeya), Kilimanjaro Islamic (Kilimanjaro), Kaizirege Junior (Kagera), Canossa (Dar), Twibhoki (Mara), Tengeru (Arusha), Marian Boysc(Pwani), Precious Bloodc(Arusha), Thomas More Machrina na Shamsiye Boys(Dar).
Shule za mwisho ni Chingungwe na Malocho (Mtwara), Nywelo(Tanga), Naputa, Chanikanguo, Mtiniko, Michiga, Masimbati, Salama na Lukokoda (Mtwara).
Watahiniwa kumi Bora kitaifa ni Teckla Haule (Canossa), Joseph Kalabwe (Kwema Modern), Mirabela Matowo (Canossa), Hamida Kihiyo (St. Aloysius Girls), Rachel Sogoja (Heritage), Clare-Anandra Hamissi, Roselyn Kissaka, Joy Kimambo, Venastra Mringo na BabyMaisara Kimazi (Feza Girls) Wasichana bora ni Teckla na Mirabela (Canossa), Hamida Kihiyo (St. Aloysius Girls), Rachel (Heritage), Clare-Anandra, Roselyn, Joy, Venastra na Baby- Maisara (Feza Girls) na Janeth Nandi (Marian Girls).
Wavulana kumi bora ni Joseph (Kwema Modern), John Bugeraha, Evance Munishi, Isack Julius, Avith Kibani, Emmanuel Dismas, Harry Mshana na Salim Mchomvu (Marian Boys), Lorian Njian (Kaizirege) na Omega Lugata (Marian Boys). Akizungumzia matokeo ya upimaji darasa la nne, Msonde alisema wanafunzi 950,167 kati ya 1,017,713 ambao ni asilimia 93.36 wamefaulu kwa kumepata Alama A, B,C na D.
Alisema wanafunzi 67,547 ambao ni asilimia 6.64 wamepata daraja E lenye ufaulu usioridhishwa.
Kuhusu ufaulu wa masomo, Msonde alisema takwimu zinaonesha kuwa wanafunzi wamefanya vizuri katika somo la Stadi za kazi, Haiba na Michezo ambapo ufaulu ni asilimia 94.67 na somo ambalo wamefaulu kwa kiwango cha chini ni Kiingereza lenye ufaulu wa asilimia 72.51.
Akiitaja mikoa iliyofanya vizuri ni Kagera, Kilimanjaro, Geita, Njombe, Iringa, Dar es Salaam, Arusha, Tanga, Mwanza na Katavi wakati halmashauri ni Bukoba Manispaa, Mji Makambako, Tanga Mjini, Chato, Mafinga Mji, Mufindi, Ilala (M), Biharamulo, Hai, Muleba.
Akitaja shule kumi bora ni St. Leo The Great na Acacia Land(Tabora), Kadama na Waja Springs (Geita), Twibhoki (Mara), Imani (Kilimanjaro), Msasa (Geita), St. Peter Claver (Kagera), Chalinze Modern Islamic (Pwani) na Mudio Islamic (Kilimanjaro).
Akizungumzia wanafunzi bora ni Loi Kitundu (Fountain of Joy), James Charles (St. Achileus Kiwanuka Emp), Erica Massaba (Tusiime), Kazungu Charles, Lightness Mpogoro, Michelle Meck, Mary Dickson na Luisa Aloyce(Waja Springs), Helieth Waryoba na Grace Manga (Twibhoki). Kwa upande wa wasichana kumi bora ni Loi (Fountain of Joy), Erica (Tusiime), Michelle, Mary na Luisa (Waja Springs), Helieth, Grace Angela Joseph (Twibhoki) na Francisca Kutageda (St. Leo The Great).
Wavulana kumi bora ni James (St. Achileus Kiwanuka Emp), Kazungu (Waja Springs), Joseph Kisinza (Msasa), James Mhele (Twibhoki), Bahati Msogela(Msasa), Steven Sige (Twibhoki), Ramadhan Issa (St Leo The Great), Augustino Alex na Jeremia Magembe (Acacia Land) na John Joseph(Twibhoki).
Aidha, Msonde alisema Baraza limefuta matokeo ya wanafunzi 58 wa Darasa la Nne na 31 wa Kidato cha Pili kutokana na kufanya udanganyifu katika upimaji na kuwa wanafunzi hao wataruhusiwa kurudia darasa na kufanya mitihani katika upimaji wa mwaka 2017.
chanzo;habarileo.

Comments