Wasichana 300 wakimbia kukeketwa.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Sihaba NkingaWASICHANA 300 kutoka mkoa wa Mara wametoroka majumbani kwao na kukimbilia kituo cha Kanisa Katoliki cha ATFG Masanga wilayani Tarime, kuepuka kukeketwa.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Sihaba Nkinga alikemea vitendo vya unyanyasaji vinavyofanywa na jamii ya Wakurya mkoani humo kwa kuwakeketa watoto wa kike, jambo linalosababisha hatari kubwa katika maisha yao.

Akizungumza katika viwanja vya kanisa hilo la Masanga, juzi, Nkinga alikipongeza kituo cha ATFG cha Kanisa Katoliki kwa kutoa elimu na mafunzo kwa watoto wa kike mkoani Mara ili kuweza kuepuka kufanyiwa vitendo vya ukeketwaji na kunusuru maisha ya wasichana hao 300.

Taarifa ya kituo hicho ilieleza kuwa kuna wasichana 300 katika kituo hicho, ambao wamekuwa wakipata mafunzo ya kujiepusha na vitendo vya kufanyiwa unyanyasaji, ukiwemo ukeketaji. Ilielezwa kuwa wasichana 47 wamehitimu mafunzo hayo.

Nkinga alisema Mara ni moja ya mikoa hapa nchini, ambayo bado inaendeleza vitendo vya unyanyasaji kwa watoto wa kike na wanawake.

“Tunaoimba jamii ya kabila la Wakurya mkoani hapa kubadilika na kuachana na vitendo hivyo vilivyopitwa na wakati vikiwemo vya ukeketaji ingawa kwasasa vitendo vya kukatana mapanga vimepungua kwa kiasi kikubwa, tunaomba vitendo hivyo viishe, wananachi waishi kwa amani wakiwemo wazee wetu,” alisema katibu huyo.

Desemba mwaka jana, ngariba wawili walikamatwa.

chanzo;habarileo.

Comments