Washindi shindano la sayansi kusomeshwa chuo kikuu.

TAASISI ya Karimjee Jivanjee (KJF) imekabidhi vyeti vya ufadhili kwa wanafunzi wa kike wawili kutoka Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mtwara kwa ajili ya kusoma masomo yao ya vyuo vikuu hadi watakapomaliza.
Ufadhili huo unatokana na wanafunzi hao kuibuka washindi wa jumla wa shindano la wanasayansi chipukizi lililoshirikisha wanafunzi takriban 300 kutoka shule  za sekondari nchini.
Wanafunzi waliopata ufadhili huo ni Diana Sosokwa na Nadhra Mresa wote wa kidato cha sita ambao mradi uliowapa ushindi ulieleza namna ya kuondoa umaskini kwa wanawake wa mkoa huo ambao walikuwa wakifika shuleni kuomba mabaki ya vyakula na nguo.
Mbali na ufadhili wa masomo, wanafunzi hao wameondoka jana kwenda nchini Ireland katika jiji la Dublin kushiriki mashindano ya wanafunzi wanasayansi chipukizi pamoja na kupata tafiti mbalimbali za kisayansi zilizofanywa na wanafunzi wa nchi hiyo ambayo itawaongezea ujuzi zaidi.
Akizungumza jana, Dar es Salaam katika hafla ya kuwaaga wanafunzi hao, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Young Scientists Tanzania (YST), ambayo inaandaa mashindano hayo hapa nchini, Dk Gosbert Kamugisha alisema shindano la wanasayansi chipukizi lilifanyika mwaka jana.
“Walitumia matatizo waliyokuwa nayo wanawake wa Mtwara wanaoizunguka shule yao na kubuni kisayansi namna ya kutengeneza mashine ya kienyeji kwa ajili ya kutotoleshea vifaranga ili wanawake hao waweze kufuga kuku ambao watawezesha kukuza kipato na kuondokana na umaskini,” alisema Dk Kamugisha.
Makamu Meneja Masoko wa KJF, Eliavera Timoth aliyesoma hotuba ya Meneja wa KJF, Devotha Rubama alisema ufadhili wa masomo kwa wanafunzi hao kwa elimu ya juu utatekelezwa pindi watakapohitimu masomo yao ya kidato cha sita.
Mkurugenzi Mtendaji wa KJF, Yusuf Karimjee alisema taasisi hiyo ina furaha kutoa mchango wao kwa wanafunzi hao kwa sababu wanaamini kuwa elimu ni muhimu kwa maendeleo ya nchi.
Alisema elimu ya sayansi pekee ndio ambayo inaweza ikatengeneza nafasi na fursa mbalimbali za kuvutia maendeleo na pia ni eneo ambalo wanafunzi wanaweza kutimiza ndoto zao.
chanzo;habarileo.

Comments