Walioiba kiwanda cha chai kukamatwa.

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali itahakikisha inawasaka wote waliohusika na upotevu wa mali za kiwanda cha chai cha Lupembe na kuwachukulia hatua.Hata hivyo, amesema serikali haitoipa nafasi migogoro yote ya uwekezaji inayopelekea wananchi kutopata ajira, bali itatatuliwa bila ya kusimamisha uzalishali.
Pia amewataka wawekezaji mbalimbali waliomilikishwa viwanda wahakikishe wanafuata kanuni na sheria ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na wananchi waweze kupata tija.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana wakati alipotembelea Kiwanda cha Chai cha Lupembe akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Njombe.
Mali za kiwanda hicho vikiwemo vipuri na vyombo vya usafiri yakiwemo malori na magari madogo 17 vilipotea baada ya Ushirika wa wakulima wa chai Muvyulu kuvamia kiwanda.
Kiwanda hicho kinakabiliwa na mgogoro kati ya mwekezaji wa kiwanda hicho, Lupembe Tea Estate na Ushirika wa Wakulima wa Chai Muvyulu ambao ameahidi kuitafutia ufumbuzi.
“Migogoro yote inayopelekea watu kutopata ajira haitapewa nafasi. Tutaisikiliza na kuipatia ufumbuzi bila ya kusimamisha uzalishaji.
Alisema serikali itayafanyia kazi maelezo yote yaliyotolewa na uongozi wa kiwanda hicho pamoja na ya wanaushirika na kisha itayatolea ufafanuzi wakati kiwanda kikiendelea na kazi.
Majaliwa alisema serikali itahakikisha mwenye haki anapata haki yake na haitakubali kuona kiwanda hicho kikisimamisha uzalishaji. Pia inafuatilia mwekezaji huyo alipataje kiwanda.
“Lupembe ni miongoni mwa viwanda ambavyo vilikufa na sasa kimeanza uzalishaji hatutakubali kife kutokana na migogoro ya wanaushirika na mwekezaji. Kiwanda hakitasimama ng’o. Hatuwezi kukubali migogoro iendelee kwani haina tija inaumiza wananchi. Najua ushirika ni wa wakulima tunataka uwe imara hatutaki ushirika wenye mizengwe mizengwe,” alisema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuja na kufanya uchunguzi wa kiwanda hicho.
Awali Waziri Mkuu alipokea taarifa ya kiwanda hicho kutoka kwa muwekezaji pamoja na taarifa ya uongozi wa Ushirika wa Wakulima wa Chai Muvyulu ambao ameahidi kuitafutia ufumbuzi.
Waziri Mkuu ameendelea na ziara yake mkoani Njombe baada ya kuikatiza Januari 22, mwaka huu na kwenda mkoani Dar es Salaam kwa shughuli za kikazi.
chanzo:habarileo.

Comments