Wakutana Roma kujadili ukeketaji.

Balozi wa Italia nchini Roberto Mengoni (katikati kushoto) akiwa na ujumbe wa Watanzania watakaohudhuria Mkutano wa Kimataifa wa Rome utakaojadili masuala mbalimbali kuhusu vita dhidi ukeketaji kwa wanawake, utakaofanyika Rome, Italia. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Uhusiano wa Taasisi ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Tanzania na Italia, Fabio Gigantino, na wa kwanza kulia ni Mbunge wa Viti Maalum; Fatma Toufiq na wa pili kulia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Kupambana na Ukeketaji Tanzania (IAC), Jennifer Chiwute. (Picha kwa Hisani na Ubalozi wa Italia).MKUTANO Mkuu wa Dunia wa kujadili namna ya kutokomeza vitendo vya ukeketaji kwa wanawake unatarajiwa kufanyika kwa siku tatu huko Rome, Italia.
Mkutano huo utakaowajumuisha wadau mbalimbali walio katika mapambano ya kutokomeza vitendo vya ukeketaji wa wanawake utaanza Januari 30 na kumalizika Februari Mosi mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa Dar es Salaam jana, Mkutano huo utakaokuwa chini ya Uenyekiti wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia Angelino Alfano utashuhudia ushiriki wa nchi 29 za Afrika, huku Tanzania ikitarajiwa kuwakilishwa na Mbunge wa Viti Maalum, Fatma Toufiq na Mwenyekiti wa Taasisi inayohusika na Utetezi wa Ukeketaji wa Wanawake (IAT) Jennifer Chiwute.
Mkutano huo utajadili kwa kina mafanikio ya kampeni ya kutokomeza vitendo vya ukeketaji wa wanawake na watoto kwa kurejea mikakati iliyowekwa, uamuzi wa kisiasa, juhudi za wanaharakati katika kutokomeza lakini pia michango inayotolewa na vyombo vya maamuzi kama Bunge na Mawaziri katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.
Akitoa maoni yake kuhusiana na mkutano huo, Balozi wa Italia nchini Tanzania, Roberto Mengoni alisema; “Italia inajumuika na mataifa mengine duniani katika vita hii ya kupinga ukeketaji kwa wanawake, vita ambayo inaelezwa na sera za ndani na nje ya nchi yetu.
“Tangu mwaka 2003, Serikali ya Italia imekuwa ikichukua hatua za kisiasa na kifedha katika kuunga mkono vita dhidi ya vitendo vya ukeketaji wa wanawake duniani kote na katika kipindi cha miaka 10 iliyopita kampeni ya kupinga vitendo hivi vya ukatili huu kwa wanawake imeonesha matunda makubwa. “Mafanikio haya yanadhihirishwa pia na hatua ya nchi 19 za Afrika kuridhia mikataba na sheria zinazopinga vitendo vya ukeketaji wa wanawake na pia kujihusisha na utoaji wa elimu kwa umma katika kujua athari ya vitendo hivyo katika jamii.” alisema
chanzo;habarileo.

Comments