Hayo yameelezwa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo mjini Dodoma wakati akijibu hoja za wajumbe wa Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Nishati na Madini, waliokutana na watendaji wa wizara hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa ya wizara hiyo, Profesa Muhongo ameongeza kuwa
katika utekelezaji wa mradi huo, serikali imepanga kuwakabidhi
makandarasi watakaotekeleza mradi huo kwa wabunge ili kuhakikisha kwamba
mradi husika unatekelezwa kikamilifu.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka
wa fedha 2016/17 bungeni mwaka jana, Profesa Muhongo alisema serikali
itafanya tathimini ya kina ya awamu ya kwanza na ya pili ya kupeleka
umeme vijijini, lengo likiwa ni kuboresha maandalizi ya utekelezaji wa
awamu ya tatu ya mradi huo.
Alisema pamoja na tathimini hiyo, masuala yatakayozingatiwa katika
awamu ya tatu ni kupeleka umeme kwenye vijiji ambavyo havikupata umeme
katika awamu ya kwanza na ya pili; kwenye viwanda vidogo vya uzalishaji
mali; na katika shule za sekondari, hospitali, zahanati, vituo vya afya,
pampu za maji na maeneo mengine muhimu ya huduma za kijamii.
Alisema awamu hiyo ya tatu, itaanza katika mwaka 2016/17 na kukamilika mwaka 2018/19.
Vijiji 8,000 vinatarajiwa kupatiwa umeme chini ya mradi wa REA Awamu
ya Tatu. Wakati huo huo, Kamati hiyo ya Bunge kupitia kwa Mwenyekiti
wake, Dotto Biteko imeipongeza Wizara ya Nishati na Madini kwa
ukusanyaji wa maduhuli kwa kipindi cha nusu mwaka na kueleza kuwa
mwelekeo wa ukusanyaji huo, unakwenda vizuri.
Awali, akiwasilisha taarifa ya wizara kuhusu upatikanaji wa fedha na
utekelezaji wa majukumu kwa kipindi cha nusu mwaka kwa Kamati, Katibu
Mkuu wa wizara, Profesa Justin Ntalikwa alieleza kuwa hadi kufikia
Desemba 31 mwaka jana, wizara ilikuwa imekusanya jumla ya Sh bilioni
201.86 sawa na asilimia 54.46 ya lengo lililokusudiwa.
“Mapato hayo yanatokana na vyanzo mbalimbali vikiwemo ada za
kijiolojia, mrahaba, ada za mwaka za leseni, mauzo ya nyaraka za zabuni,
mauzo ya gesi asilia, tozo ya mauzo ya umeme na shughuli za utafiti wa
mafuta na gesi asilia,” alieleza Profesa Ntalikwa.
Akieleza utekelezaji wa majukumu ya wizara kwa kipindi cha Julai hadi
Desemba mwaka jana, Katibu Mkuu alisema serikali imeendelea kutekeleza
miradi mbalimbali ya kimkakati kulingana na mpango wake na kuitaja
miradi kadhaa ikiwemo Mradi wa Kusafirisha Umeme Msongo wa kilovoti 400
kutoka iringa hadi Shinyanga uliokamilika Desemba 28, 2016.
“Mradi wa Kinyerezi II wenye Megawati 240 utekelezaji wake umefikia
asilimia 29 na Serikali imekwishatoa mchango wake wote wa asilimia 15
sawa na shilingi bilioni 110 na mradi huu unategemewa kukamilika mwaka
2018,” alisisitiza Profesa Ntalikwa.
Akizungumzia Mradi wa Kinyerezi I, Extension ya Megawati 185 ambao ni
mwendelezo wa upanuzi wa Mradi wa Kinyerezi 1, ameeleza kuwa, mradi huo
unaendelea kutekelezwa na unatarajiwa kukamilika mwaka 2018.
Akizungumzia uendelezaji wa uchimbaji mdogo, Profesa Ntalikwa alisema
ili kukuza utendaji wao, wizara inaendelea na hatua za uanzishwaji wa
vituo vya mfano vitano katika wilaya za Kilwa, Mpanda, Chunya na Bukoba
kwa ajili ya wachimbaji wadogo; ambavyo vitatumiwa na wachimbaji hao
kuchenjua madini yao na kujifunza namna bora ya kuendesha migodi yao
kitaalamu na kwa tija zaidi.
Ahadi ya Waziri Mkuu Akizungumza na watendaji wa idara za serikali
wilayani Longido katika ziara yake ya kikazi mkoani Arusha Desemba mwaka
jana, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema serikali imesaini mkataba
kwa ajili ya kukamilisha kuweka umeme katika vijiji 8,000 vilivyosalia
katika awamu ya kwanza na ya pili ya Mradi wa Umeme Vijijini (REA).
Alisema wakandarasi walishasaini mikataba hiyo na kwamba mwezi Aprili 2017, vijiji hivyo vitakuwa vimeshapata umeme.
Alisema maeneo ambayo umeme huo hautafika, wananchi watafungiwa
nishati ya umeme wa jua kwa gharama ile ile ya Sh 27,000, ambayo ni sawa
na gharama za umeme wa gridi ya taifa. Waziri Mkuu alisema baada ya
miradi hiyo kukamilika, vijiji vyote nchini vitakuwa na umeme.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, umeme huo utawezesha wananchi kujikwamua
na hali ngumu ya maisha kwa kubuni miradi mbalimbali ya uzalishaji mali
katika maeneo yao.
Muhongo akiwa Mara Kwa upande wake, Profesa Muhongo alisema vijiji
vyote ambavyo havijafikishiwa huduma ya umeme, vitapata huduma hiyo
kupitia mradi mkubwa wa umeme vijijini Awamu ya Tatu unaotekelezwa na
REA.
Alisema hayo katika ziara yake mkoani Mara mwaka jana, kukagua
utekelezaji wa mradi wa umeme vijijini Awamu ya Pili (REA II) ambao
unamalizika.
Alisema katika maeneo mbalimbali aliyotembelea, alielezwa kuwa vijiji
vya ndani, havina umeme kwani nishati hiyo imeishia kwenye vijiji
vilivyopo katika barabara kubwa na kwenye vituo vya biashara. Alisema
serikali inatambua vijiji ambavyo havikufikishiwa huduma hiyo, hivyo
aliwaomba wananchi katika vijiji hivyo kuwa na subira.
Alisema mradi wa REA III umetengewa zaidi ya Sh trilioni moja, ambayo
ni mara tatu zaidi ya iliyotengwa katika mradi wa REA II ambao
unamalizika kwa kuunganisha baadhi ya vijiji.
chanzo;habarileo.
Comments