UN yatahadharisha kuhusu hali mbaya katika kanda ya Ziwa Chad.

Jumuiya za misaada ya kibinadamu za Umoja wa Mataifa zimetangaza kuwa, zaidi ya watu milioni 11 wakazi wa eneo la Ziwa Chad wanahitaji misaada ya dharura.

Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa katika kanda ya Ziwa Chad, Toby Lanzer ametahadharisha kuwa eneo hilo linasumbuliwa na uhaba mkubwa wa chakula na kwamba wakazi wengi wa eneo la Ziwa Chad wanaishi katika hali ngumu.
Ripoti zinasema kuwa karibu watu milioni mbili na nusu wakiwemo wanawake na watoto wengi katika nchi za kanda ya Ziwa Chad wamelazimika kukimbia miji na vijiji vyao kutokana na mashambulizi ya kundi la kigaidi la Boko Haram. 
Ripoti hizo zinasema kuwa, asilimia 80 ya wakimbizi hao wamepewa hifadhi katika nyumba za ndugu na jamaa zao, suala ambalo limezidisha mashinikizo ya kiuchumi kwa watu wa eneo hilo.
Toby Lanzer amesema kuwa Umoja wa Mataifa unafanya jitihada za kushirikiana na nchi za Cameroon, Nigeria, Chad na Niger kwa ajili ya kutafuta njia ya kukomesha mgogoro huo mkubwa wa kibinadamu ambao umesababishwa na mashambulizi na uharibifu unaofanywa na kundi la Boko Haram.
Zaidi ya watu elfu 20 wameuawa na mamilioni ya wengine kulazimika kuwa wakimbizi tangu kundi la kigaidi la kiwahabi la Boko Haram lianzishe mashambulizi ya kiholela kaskazini mwa Nigeria mbayo sasa yamevuka mipaka na kuingia katika nchi jirani kama Cameroon na Chad.
chanzo:parstoday.

Comments