Afisa wake wa mawasiliano Sean Spicer amesema hatua hiyo ya rais
inaonesha kwamba “anataka kuwatetea Wamarekani wote, wakiwemo wale ambao
hawajazaliwa.”
Agizo hilo ambalo kirasmi linafahamika kama “the Mexico City Policy”
(Sera ya Jiji la Mexico) huenda likayakera makundi ya kutetea uhuru wa
wanawake kuamua kuhusu uzazi, ambayo tayari yametiwa wasiwasi na msimamo
wake wa kupinga utoaji mimba.
Bw Trump anaunga mkono utoaji mimba upigwe marufuku Marekani.
Lakini hii si mara ya kwanza kwa marufuku dhidi ya ufadhili wa mashirika ya utoaji mimba nje ya Marekani kutolewa.
Rais wa Republican Ronald Reagan mara ya kwanza alianzisha Sera ya
Jiji la Mexico mwaka 1984 na kuwa wa kwanza kupiga marufuku ufadhili
huo.
Lakini chama cha Democratic kilibatilisha marufuku hiyo chini ya utawala wa Bill Clinton.
Sera hiyo inayataka mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo yanapokea
ufadhili wa serikali ya Marekani kukubali “kutotekeleza na kutoendeleza
au kutohamasisha watu watumie utoaji mimba kama njia ya uzazi wa mpango
katika nchi nyingine”.
Kwa miongo mingi, imekuwa kwamba pesa za Marekani haziwezi kutumiwa katika utoaji mimba katika mataifa ya nje.
Mwaka 2009, Barack Obama alisitisha utekelezaji wa sera hiyo, ambayo ilikuwa imrejeshwa chini ya utawala wa Rais George Bush.
Makundi ya kutetea uhuru wa wanawake kuamua kuhusu uzazi wamepinga hatua hiyo ya Bw Trump.
“Ni jambo la kusikitisha sana kwamba moja ya hatua za kwanza za Trump
inaunganisha mambo mawili kwa pamoja: kunyamazisha wote wanaotofautiana
naye na kuwakandamiza wanawake,” taarifa kutoka kwa kundi la Naral
Pro-Choice America imesema.
“Siku mbili baada ya maandamano ya kihistoria ya wanawake ya kumpinga
Trump kufanyika na siku moja baada ya maadhimisho ya uamuzi wa
kihistoria wa mahakama kesi ya Roe v. Wade, Donald Trump anapatia
kipaumbele hatua ya kurejesha … sera ambayo inawanyamazisha wahudumu wa
afya na kuweka hatarini wagonjwa.”
Wakati wa kampeni, Bw Donald Trump, ambaye awali alitetea uhuru wa
wanawake kuamua kuhusu uzazi, aliambia MSNBC kwamba “lazima kuwe na aina
fulani ya adhabu kwa mwanamke” iwapo utoaji mimba utakuwa marufuku.
Baadaye, aliondoa tamko hilo baada ya kushutumiwa vikali na makundi ya kutetea haki za wanawake.
Maafisa wa kampeni wa Bw Trump walisema waliamini uamuzi kuhusu
uhalali wa utoaji mimba unafaa kuachiwa majimbo yenyewe, na kwamba
adhabu inafaa kutolewa kwa wanaotoa huduma za utoaji mimba.
Alisema anaunga mkono marufuku ya utoaji mimba ila tu wakati mimba
imetokana na “ubakaji, kujamiiana kwa maharimu au wakati maisha ya mama
yamo hatarini”.
Bw Trump pia ameahidi kujaza nafasi ya jaji iliyo wazi Mahakama ya Juu na jaji ambaye ni mhafidhina kuhusu masuala ya kijamii.
Hayo yakijiri, Bunge la Congress limeashiria nia yake ya kuondoa
ufadhili wa serikali kwa kundi la Planned Parenthood, kundi linalotoa
huduma za afya ya uzazi Marekani na nje ya taifa hilo.
chanzo: zanzibar24
Comments