Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba ametoa kauli hiyo
ya serikali mjini Kigoma wakati wa uteketezaji wa silaha haramu,
lililofanyika kikanda mkoani Kigoma, na kueleza kuwa kwa sasa hakuna
tena wakimbizi watakaoingia kwa makundi watakaoruhusiwa kuingia nchini.
Mwigulu alisema serikali itawapokea wakimbizi mmoja mmoja na kila
atakayeingia atahojiwa na mamlaka zinazohusika na mamlaka zikijiridhisha
kuwa anastahili hadhi ya ukimbizi, atapokewa na kupelekwa kwenye kambi
za wakimbizi zilizopo, kwani hakuna tena kambi ya wakimbizi
itakayofunguliwa kwa sasa.
Alisema serikali kwa kutumia vyombo vyake, imejiridhisha kwamba
hakuna hali mbaya ya usalama, inayowakimbiza raia hao kutoka kwenye nchi
zao na kwamba zaidi imegundulika kuwa wengi wao wanakimbia kwa sababu
za kiuchumi, kuja kutafuta namna ya kuishi ili kukidhi hali zao za
maisha.
Alisema uwepo na uingiaji wa wakimbizi nchini, umekuwa na mchango
mkubwa katika uzagaaji wa silaha haramu sanjari na kuongezeka kwa
matukio ya utumiaji wa silaha na kuathiri uchumi na maisha ya watu
mbalimbali.
Katika hatua nyingine, waziri huyo amesema serikali imefuta utaratibu
wa kutoa uraia kwa makundi, kama ilivyofanya kwa wakimbizi wa Burundi
waliopo nchini. Alisema kwamba kwa sasa uraia utatolewa kwa mtu
kulingana na maombi yake.
Alisema ukarimu huo wa Watanzania, umekuwa na athari kubwa katika
ulinzi na usalama nchini, hasa mikoa ambayo imewahifadhi watu hao
kutokana na kuongezeka kwa vitendo vya mauaji, ujambazi wa kutumia
bunduki, lakini kupanda mbegu mbaya ya kuuana kwa kulipiza visasi
ambavyo vimekuwa vikifanywa na raia hao waliopewa uraia.
“Kwa mamlaka niliyopewa, natoa amri ya kusimamisha kutoa uraia kwa
makundi kama ambavyo imetoa Tanzania na haijawahi kutokea nchi nyingine,
tumeona athari kubwa ya watu hao na sasa sehemu kubwa ya Mkoa wa Tabora
imekuwa na hali mbaya kiusalama na tabia ya kulipizana visasi,”
alieleza Mwigulu.
Akitoa taarifa kwa waziri, Kamishna wa Mafunzo na Operesheni wa Jeshi
la Polisi, Marijani Nsato alisema silaha haramu 5,608 zikiwemo bunduki
za kivita, zilitarajia kuteketezwa. Nsato alisema katika silaha hizo,
kulikuwa na bastola 21, Shortgun 606, SMG 166, Riffle 300, bastola
bandia 21, FN Riffle 3, G3 moja, SAR 3 na magobore 4487.
Sanjali na bunduki hizo, aliitaja mikoa ambayo imeshiriki katika
kuchangia bunduki haramu zilizoteketezwa kuwa ni Kagera 100, Rukwa 189,
Katavi 81, Simiyu 16, Mwanza 88, Geita 82, Mara 80 na Kigoma ukiwa na
jumla ya bunduki 424 ambazo zimeteketezwa katika kazi ya jana.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Emmanuel Maganga alisema
mkoa huo kuwa mpakani na kupokea idadi kubwa ya wakimbizi kutoka nchi za
Maziwa Makuu, kumechangia mkoa huo kuathirika kwa kiasi kikubwa na
uzagaaji silaha haramu na matukio ya ujambazi kwa kutumia silaha.
Alisema mkoa utaendelea kuweka mkakati wa kudhibiti silaha haramu na matukio ya ujambazi wa kutumia silaha.
chanzo;habari;eo.
Comments