Dk. Shein aliyasema hayo leo mara baada ya kufanya ziara ya
kutembelea kiwanda hicho akiwa amefuata na Wajumbe wa Baraza la
Mapinduzi pamoja na watendaji wakuu wa Serikali wakiongozwa na Katibu
Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahaya
Mzee.
Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa ziara hiyo aliyoifanya
akiwa na viongozi wengine wa Baraza la Mapinduzi na Watendaji Wakuu wa
Serikali ni ushauri wake wa kuwataka viongozi hao washiriki pamoja ili
wapate kujua muelekeo, hatma, nyenzo, wafanyakazi, mambo yanayohitajika
pamoja na changamoto zilizopo.
Akiwa katika ziara yake ya mwanzo ya kikazi tokea kuingia mwaka mpya
wa 2017, Dk. Shein alisema kuwa tokea kuanzishwa Kiwanda hicho mnamo
mwaka 1966 haikupiga hatua kubwa licha ya juhudi kubwa zilizochukuliwa
na Serikali kwa mashirikiano ya Serikali ya China na baadae mnamo mwaka
1980 Serikali ya Uholanzi kuziunga mkono ikiwemo kukijengea uwezo wa
kiufundi na kiutawala.
Dk. Shein alisema kazi ya kikiendeleza Kiwanda hicho si ndogo lakini
akimnukuu shujaa wa Ufaransa Napoleon Bonaparte, aliekuwa kiongozi wa
kwanza wa nchi hiyo tokea kufanyika kwa Mapinduzi ya mwaka 1799
alivyosema kuwa “Tulikwenda, Tukaona na Tukashinda”, basi anaamini
mafanikio yatapatikana baada ya ziara hiyo.
“Tumekuja, tumeona na tutashinda lakini kubwa ni mashirikiano ya
pamoja kati ya Serikali na wafanyakazi wa Kiwanda hichi…tujiandae kubwa
lijalo”,alisema Dk. Shein.
Hivyo, Dk. Shein alisisitiza kuwa kazi ya kukiendeleza Kiwanda hicho
ni ya Serikali peke yake bali inahitaji mashirikiano makubwa kutoka kwa
wafanyakazi wa Karakana hiyo kwani hilo linatasidia kwa kiasi kikubwa
kufikia lengo lilolokusudiwa.
Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa Serikali inaweza kufanya wajibu wake
katika kuhakikisha Kiwanda hiyo inarudi katika uhalisia wake lakini bila
ya mashirikiano ya wafanyakazi wa karakana hiyo lengo halitofikiwa.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa yeye na ujembe aliofuatana
nao wameona waliyoyaona katika kiwanda hicyo zikiwemo changamoto
zilizopo pamoja na zile za wafanyakazi wake na serikali itafanya juhudi
ya kuangalia nini kitafanyika na baadae taarifa rasmi itatolewa.
Hata hiyo, Dk. Shein alisisitiza haja ya kutofanya kazi kwa mazoea
kwa kuutaka uongozi na wafanyakazi wa Kiwanda hicho kuyaweka vizuri
mazingira ya Kiwanda hicho pamoja na kuviweka vifaa vichakavu katika
utaratibu maalum ambapo licha ya changamoto zilizopo lakini Kiwanda
hicho kinaweza kuvutia iwapo hatua hizo zitachukuliwa.
Nae Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Hamad Rashid
Mohammed alitoa shukurani za pekee kwa Rais Dk. Shein kwa ziara yake
hiyo ya mara ya pili katika Kiwanda hicho na kueleza jinsi Dk. Shein
anavyofanya maamuzi yake kwa mashirikiano kati yake na wasaidizi wake na
hakurupuki katika hilo.
Waziri Mohammed alisema kuwa juhudi za makususdi zimekuwa
zikichukuliwa na Wizara yake katika kuhakikisha wakulima wanatatuliwa
changamoto zinazowakabili ikiwa ni pamoja na kuwalimia mashamba yao kwa
kutumia matrekta ambapo katika msimu huu tayari asilimi 87 ya mabonde
yameshalimwa licha ya uhaba wa vitendea kazi huku akieleza changamoto ya
Taasisi kama hiyo kuwa Kitengo.
Nao wafanyakazi wa Kiwanda hicho katika risala yao iliyosomwa na Mkuu
wa Kitengo cha zana za Kilimo, Mohammed Omar Mohammed walisema kuwa
wanajivunia ujio wa Rais kwa mara ya pili katika kipindi cha takriban
miaka mitatu kwa lengo la kujali kazi ambazo Karakana hiyo
inazitekeleza.
Mkuu huyo wa kitengo alieleza historia ya Karakana hiyo, hali halisi
ya sasa , majukumu yake ya kuratibu kazi zote zinazohusiana na zana za
kilimo huku wakieleza kuwa kiwanda hicho kinatoa huduma za kiufundi kwa
zana zote za kilimo za Serikali na za wateja binafsi pamoja na huduma
za ufundi ambazo haziusiani na zana za kilimo kwa taasisi za Serikali.
Wakieleza miongoni mwa majukumu ya Kiwanda hicho ni pamoja na
kuendesha mafunzo ya amali ya kiufundi ya nadharia na vitendo kwa vijana
ambao wanapenda kupata ujuzi wa kiufundi hasa kwenye fani za umeme na
umakanika kwa muda wa miaka miwili.
Sambamba na hayo, wafanyakazi hao walieleza changamoto mbali mbali
zinazowakabili Kiwandani hapo ambapo mapema Dk. Shein aliitembelea
Kiwanda hicho na kupata maelezo kutoka kwa Wakuu wa Vitengo ambao
walieleza changamoto zilizopo ambapo nayeye alitumia fursa hiyo kuuliza
masuala kadhaa.
Mnamo mwaka 1966, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilipata msaada wa
matrekta 50 kutoka Jamhuri ya Watu wa China pamoja na majembe yake ya
kuchimba na kuburuga kwa lengo la kuwapunguzia mzigo wakulima ambao
walikuwa wakilima kwa kutumia jembe la mkono.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
chanzo; zanzibar24.
Comments