RC- Wizara isitoe vibali kuuza mahindi nje.

MKUU wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ameishauri Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kuacha kutoa vibali kwa wafanyabiashara nchini kusafirisha mahindi nje ya nchi.
Gambo alisema hayo jana baada ya kutembelea maghala matatu ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Kanda ya Arusha.
Alisema uongozi wa mkoa wa Arusha ulishapiga marufuku uuzwaji wa mahindi nje ya nchi lakini kuna baadhi ya wafanyabiashara wamekamatwa na vyombo vya ulinzi na usalama wakiwa na vibali kutoka wizarani vinavyowaruhusu kupeleka mahindi nchi jirani ya Kenya.
Alisema kutokana na mkanganyiko huo aliwaomba watendaji wa Wizara kuacha kutoa vibali kwa wafanyabiashara kuuza mahindi nje ili kuwasaidia wenye viwanda vya nafaka kuuza unga na pumba nje ili nao waweze kupata faida na nchi iweze kupata faida zaidi.
Gambo alisema mbali ya hilo pia serikali mkoani humo imefanikiwa kuziba njia za panya zilizokuwa zikitumika na wafanyabiashara kutorosha mahindi kwenda nchi jirani ya Kenya.
“Vibali vya Wizara kwa wafanyabiashara kuuza mahindi nje vinatuchanganya na vinapingana …tunaiomba wizara iache kufanya hivyo kwa maslahi ya nchi na wafanyabiashara wa ndani ili waweze kuuza unga badala ya mahindi kwani watanufaika zaidi,’’ alisema Gambo.
Meneja wa NFRA Kanda ya Arusha, Abdillah Nyangasa alikitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa, alisema kuwa kazi ya ununuzi iliyoanza Agosti 25 mwaka jana na kumalizika Novemba 30 mwaka huo malengo yalikuwa kununua mahindi tani 15,000 lakini walifanikiwa kununua mahindi tani 5,111 tu na hiyo ni kutokana na ufinyu wa bajeti.
chanzo;habarileo.

Comments