Amesema hatua hiyo itapunguza vifo na majeruhi katika migogoro ya wakulima na wafugaji mkoani humo.
Alitoa ombi hilo kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu
Nchemba katika mikutano ya hadhara katika vijiji vya Tindiga na Dumila.
Kwa upande wake, Nchemba alisema kuanzia jana ikitokea mkulima ama mtu
yeyote amejeruhiwa kwa sime, panga, mkuki au mshale mkoani Morogoro,
serikali itafuta sheria inayoruhusu watu kutembea na silaha.
Alisema hatua hiyo inatokana na ombi la Mkuu wa Mkoa, Dk Kebwe la
kufuta au kurekebisha sheria hiyo ili kupunguza vifo na majeruhi katika
migogoro ya wakulima na wafugaji.
Aidha, waziri huyo ameunda tume itakayokuwa na jukumu la
kuwaorodhesha viongozi wa serikali wa ngazi mbalimbali wilayani Kilosa
mkoani Morogoro, wanaodaiwa kwenda kinyume na sheria ya utendaji kazi.
Majina yao yatawasilishwa ofisini kwake kwa ajili ya kuchukuliwa hatua
za kisheria.
Alitoa kauli hizo kwa nyakati tofauti wilayani Kilosa jana,
alipozungumza na viongozi wa Serikali ya wilaya hiyo na mkoa,
wakiongozwa na Dk Kebwe.
Aliwaambia wafugaji na wakulima kuwa hakuna sababu yoyote ile,
itakayosababisha mtu kuchukua hatua za kumuua binadamu mwezie, kwani
uhai haulinganishwi na thamani ya kitu chochote kile. Aliwaonya viongozi
wa ngazi mbalimbali, kuacha urafiki na wauaji.
Alisisitiza kiongozi yoyote atakayebainika kuwa na ushirikiano na muuaji, basi na yeye ataunganishwa kwenye kesi ya mauaji .
Waziri Nchemba alivitaka vyombo vya dola na vya kisheria, kutosubiri
wananchi wachukue sheria mkononi, bali wachukue sheria na adhabu
inayostahiki wote wenye kutenda makosa ili kuhakikisha vitendo hivyo
vinakomeshwa mara moja.
“Duniani kote sheria isipochukua mkondo wake kwa wahalifu, basi
wananchi watachukua sheria mkononi“ alisema. Aliwataka wafugaji kukutana
na kujadili wao wenyewe namna ya kuacha tabia hizo.
Alisema kwa yule atakayefanya mauaji au kujeruhi, basi wafugaji
wenzake wawe wa kwanza kumkamata na kufikisha kwenye vyombo vya sheria.
Aliwaonya wakulima kuwa atakayechukua hatua za kumuua mfugaji kwa sababu
ya kulisha shamba, basi naye atafikishwa mahakamani na kupewa adhabu
kali.
Aliwataka wakulima kutolipiza visasi kwa yote yaliyotokea, kwani
watuhimiwa wote wameshakamatwa na kufikishwa mahakamani na watakuwa
mfano kwa wengine .
“ Nimesikia kuwa wafugaji wanafanya mauaji kwa makusudi kutokana na
viburi vyao kwa kigezo watauza mifugo yao ili washinde kesi, kama
wamezoea hivyo, basi watafilisika na mifugo yao na jela watakwenda “
alisema.
Dk Kebwe alisema pamoja na wafugaji wengi kutembea na silaha, chanzo
kingine cha migogoro ya wakulima na wafugaji ndani ya wilaya na mkoa huo
ni viongozi wa ngazi za vijiji, kupokea rushwa na kuwakaribisha
wafugaji maeneo ya vijiji vya wakulima kinyume cha sheria.
“Nimeanza kuchukua hatua za kuwachunguza viongozi wote wa vijiji na
kata zenye migogoro na watakaobainika kuhusika na vitendo vya kinyume
cha sheria, watawajibishwa mara moja,” alisema Dk Kebwe.
Akijibu ombi la mkuu wa mkoa, Waziri Nchemba alisema kuwa kuanzia
jana, iwapo kutatokea tukio lolote la mkulima au mtu yoyote kuchomwa
mkuki, mshale, sime au kupingwa fimbo mtu, basi Serikali kupitia wizara
yake itaifuta sheria ya kutembea na silaha.
Pamoja na kutoa tishio hilo, waziri aliwaonya wananchi wenye tabia ya
kutaka fedha kwa njia haramu, kwa kushikilia mifugo ya wafugaji.
Alisema kuna watu wamekuwa wakishikilia mifugo ya wafugaji bila kosa
lolote ili tu wapate fedha. Alitaka vitendo hivyo, vikomeshwe mara moja.
“Tukio kama hili si migogoro ya ardhi, bali ni ujambazi sawa na
uhalifu mwingine , na watu wa aina hii washughulikiwe kisheria ili
kukomesha tabia hizo” alisema Nchemba. Waziri Nchemba alitembelea wilaya
ya Kilosa kwa lengo la kutatua changamoto za migogoro ya wakulima na
wafugaji.
chanzo;habarileo.
Comments