Akizungumza katika mkutano wa hadhara kijijini hapo, Mkuu wa Mkoa,
Rugimbana alisema, kijiji hicho kina mpango wa ardhi wa siku nyingi,
hivyo ni vema ukazingatiwa na kufuatwa badala ya watu kuvamia maeneo
kiholela.
Mkuu wa mkoa huo alisema, amri iliyotolewa na wakuu wa wilaya hiyo
waliotangulia, inabaki vivyo hivyo, hakuna shughuli zozote kuendelea
katika eneo hilo ambalo linagombaniwa hadi kamati iliyoundwa na wilaya
ambayo mkoa utaongeza watu wake itakapokamilisha uchunguzi wake.
“Marufuku kufanya shughuli zozote katika eneo hilo, hadi kamati
iliyoundwa na viongozi wa wilaya ambayo mimi nitaongezea watu,
itakapokamilisha uchunguzi,” alisisitiza.
Alisema waliovamia maeneo hayo, kabla ya kuwaita wavamizi au kabla ya
kuwachukulia hatua, wanatakiwa kujisajili kwa viongozi wa kijiji
wanaohusika, kupitia mikutano ya hadhara, wasipofanya hivyo,
watawahesabiwa kuwa ni wavamizi wa maeneo ya kijiji hicho na hawana nia
nzuri.
Huku akishangiliwa na wananchi, Mkuu wa Mkoa alisema, maeneo hayo
yamevamiwa na watu ambao sio wa kijiji au kata ya Makanda, wamechukua
maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wafugaji na kuyabadili kuwa ya kilimo.
Akizungumza kwa msisitizo alisema, waliovamia maeneo hayo ni wahuni
wachache kutoka nje ya eneo hilo, na kusababisha vurugu miongoni mwa
wananchi na kuvuruga mpango ardhi wa kijiji kwa kutoa fedha kidogo ili
kupata maeneo hayo.
Mkuu wa Mkoa aliwataka wazee wa kijiji hicho kumsaidia katika
kuhakikisha amani inadumu kijijini hapo, akawataka kwanza waunde Baraza
lao ili kusaidiana na madiwani katika kuhakikisha wanasimamia amani
kijijini hapo.
Diwani mstaafu wa Kata ya Makanda, Anthony Lyamunda, alimsifu Mkuu wa
Mkoa wa Dodoma kufika kijijini hapo kwani wamekuwa wakisumbuliwa na
watu wanaoitwa vishoka kutokana na vitendo vya kuvamia ardhi wanaotaka
kubadili matumizi ya ardhi kijijini hapo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Makanda, Msafiri Makacha, wakati akifunga
mkutano huo, alimweleza Mkuu wa Mkoa kwamba kamati iliyoundwa na
viongozi wa wilaya inaanza kazi leo (jana) kutatua mgogoro wa ardhi, ana
hakika watapata ufumbuzi wa kudumu juu ya suala hilo.
chanzo:habarileo.
Comments