Mwenyekiti CCM apigwa risasi.

Image result for ccmMWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mbeya Mjini, Ephraim Mwaitenda (60) amenusurika kifo baada ya kupigwa risasi na mtu asiyefahamika akiwa amelala nyumbani kwake wilayani Kyela.
Akizungumzia tukio hilo, Kaimu Katibu wa CCM Mkoa wa Mbeya, Zongo Lobe alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana, ambako mtu asiyefahamika alimvizia Mwaitenda alipokuwa amelala na kisha kuchana nyavu ya dirisha kisha kumpiga risasi.
Zongo alisema kiongozi huyo baada ya kupigwa risasi hiyo, awali hakutambua kuwa amepigwa risasi na badala yake alihisi kuwa ni simu yake imelipuka na kwamba alijikuta ameanguka chini, lakini akiwa anajitambua.
Alisema baada ya kuinuka ili arudi kitandani, ndipo alipobaini kuwa katika mgongo wake kuna sehemu kuna jeraha na damu zinachuruzika, hivyo akamuomba dada yake aliyekuwa amelala chumba cha pili amsaidie na ndipo walipoanza kuhisi harufu ya baruti ndani ya chumba hicho.
Alifafanua kuwa mwenyekiti huyo alikuwa ameenda Kyela kwa shughuli za kilimo, alikuwa anapanda mpunga ambako siku nzima ya juzi aliitumia kufanya shughuli hiyo.
“Alinipigia mwenyewe simu na kunijulisha kuwa amepigwa risasi na watu wasiofahamika, na kwa sababu ilikuwa usiku niliamua kumpigia simu mkuu wa mkoa kwa ajili ya kumjulisha, lakini akanijibu kuwa alikuwa tayari ameshapata taarifa na ameagiza vyombo vya dola kufuatilia,” alisema Zongo.
Alisisitiza kuwa yeye kama kiongozi wa chama Mkoa hawezi kulihusisha tukio hilo na jambo lolote na badala yake wanaliachia Jeshi la Polisi kufuatilia na kuchukua hatua.
Hata hivyo, Zongo aliliomba jeshi hilo pamoja na vyombo vingine vya dola, kuhakikisha wahusika wa tukio hilo wanapatikana na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Kaimu Kamanda wa Polis Mkoa wa Mbeya, Emmanuel Lukula alithibitisha tukio hilo na kueleza kuwa lilitokea katika kitongoji cha Ilopa, Kijiji cha Mahenge Kata ya Makwale wilayani Kyela ambako ndiko nyumbani kwa kiongozi huyo.
Kamanda Lukula alisema Mwaitenda alijeruhiwa sehemu ya mgongoni, ambako pana jeraha lililosababisha kuvuja damu nyingi, hali iliyosababisha aanze kuishiwa nguvu.
Alieleza kuwa kiongozi huyo alikimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kyela na ilipofika asubuhi alihamishiwa katika Hospitali ya Kanda ya Rufaa ya Mbeya, ambako anaendelea na matibabu.
chanzo:habarileo.

Comments