Mawaziri hao waliyasema hayo kwa nyakati tofauti wakati wakizungumza
na waandishi wa habari kuhusu undani wa mikataba waliyoisaini juzi
wakati wa ziara ya Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan iliyomalizika
juzi jioni.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy
Mwalimu alisema katika mkataba aliousaini utawezesha ushirikiano baina
ya nchi hizo mbili katika sekta ya afya ikiwemo ujenzi wa kiwanda cha
dawa.
Aidha, alisema kupitia mkataba huo, pia nchi hiyo ya Uturuki
itawezesha mafunzo ikiwemo kubadilishana uzoefu kwa madaktari bingwa wa
magonjwa sugu kama vile figo, saratani na moyo, hali itakayoongeza idadi
ya madaktari bingwa nchini waliobobea katika kutibu magonjwa hayo.
“Lakini pia watatusaidia kupata mafunzo ya kutumia katika hospitali
zetu mfumo wa udhibiti wa taarifa za hospitali (HMIS) ambao ni wa
kieletroniki unaotumika kuhifadhi taarifa zote za wagonjwa na takwimu za
wagonjwa wa magonjwa mbalimbali,” alifafanua Ummy.
Alisema kupitia mfumo huo, kwa sasa itakuwa ni rahisi Serikali kupata
takwimu ya magonjwa mbalimbali kama vile kifua kikuu na moyo lakini pia
mfumo huo utarahisisha katika eneo la ukusanyaji mapato kwa kuwa mfumo
mzima uko wazi.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alisema
mkataba aliousaini umelenga katika kuikuza sekta ya utalii nchini ambapo
nchi hizo mbili zote kwa pamoja zitakuwa na ushirikiano katika
kutangaza utalii unahusu pande zote mbili.
“Lakini pia tutabadilishana wataalamu kwa lengo la kujifunza na
kuongeza ujuzi katika eneo la sekta ya utalii, tutaangalia namna wenzetu
walivyofanya hadi kufanikiwa kuvutiwa idadi kubwa ya watalii kuliko
sisi ambao tuna vivutio vingi vya utalii lakini tunapokea watalii
wachache,” alifafanua.
Alisema kwa takwimu zilizopo Uturuki inapokea watalii takribani
milioni 10 kwa mwaka wakati Tanzania inapokea kwa sasa watalii milioni
moja kwa mwaka pekee.
Naye Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi,
Stella Manyanya alisema amesaini mkataba wa ushirikiano baina ya
Tanzania na Uturuki katika eneo la kubadilishana uzoefu kwenye kilimo.
Alisema Uturuki ni nchi ya saba duniani katika kuzalisha mazao ya
kilimo na kwa kuwa Tanzania takribani asilimia 80 ya wakazi wake
wanajishughulisha na kilimo, hiyo ni fursa nzuri ya kuikuza sekta hiyo
kwa manufaa ya taifa na wananchi kwa ujumla.
Aidha, alisema kwa upande wa teknolojia, nchi hiyo ni moja ya kati ya
nchi zinazoongoza duniani katika masuala ya teknolojia hivyo kupitia
mkataba huo, Tanzania itanufaika kwa kupata mafunzo mbalimbali katika
eneo hilo la teknolojia.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, kupitia
mkataba aliousaini wamekubaliana kushirikiana na nchi hiyo katika eneo
la kuendeleza viwanda ambapo nchi hiyo itaanzisha viwanda mbalimbali
hapa nchini kikiwemo kiwanda cha nguo.
Aidha alisema kupitia mkataba wa Shirika la Maendeleo ya Viwanda
vidogo (SIDO) na shirika la viwanda vya Kati Uturuki, mkataba huo
unahusu makubaliano ya kupatiwa mafunzo, ikiwa ni pamoja na
kubadilishana wataalamu kwa lengo la kuongeza ujuzi na uzoefu.
Mikataba iliyosainiwa ni pamoja na mkataba wa ushirikiano baina ya
Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) na shirika la ndege Uturuki,
ushirikiano baina ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na Shirika la
Utangazaji Uturuki na mkataba wa ushirikiano katika maendeleo baina ya
nchi hizo mbili.
Mikataba mingine ni pamoja na ushirikiano katika sekta ya elimu na
utafiti, ushirikiano baina ya Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) na
Shirika la Viwanda vya Kati Uturuki na ushirikiano katika sekta ya
Utalii kwa nchi zote mbili.
Pia mikataba mingine iliyosainiwa mbele ya marais hao ni ushirikiano
katika viwanda na ulinzi, ushirikiano kwenye sekta ya afya na
ushirikiano baina ya chuo cha Diplomasia cha Tanzania na cha Uturuki.
chanzo;habarileo.
Comments