Kwa mujibu wa taarifa ya Benki ya Dunia ofisi ya Tanzania, Diop atafanya mazungumzo na viongozi wakuu nchini akiwamo Rais John Magufuli, pamoja na maofisa wengine wa juu wa serikali akiwamo Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Profesa Benno Ndulu.
Pia atakutana na wawakilishi wa sekta binafsi na asasi za kijamii. Kwa sasa, Benki ya Dunia inasaidia miradi 27 nchini yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 4.2 katika mikoa mbalimbali ambako Tanzania inafadhili kwa dola za Marekani milioni 551, hivyo kufanya jumla ya thamani kuwa dola bilioni 4.75.
Ukubwa wa msaada huo (asilimia 22) ni katika sekta ya usafirishaji ikifuatiwa na maendeleo ya mijini 20%.
Wakati wa ziara ya Diop, Rais Magufuli anatarajiwa kuzindua rasmi Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka jijini Dar es Salaam (DART) ambao unafadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia Mradi Mkuu wa Pili wa Usafirishaji (CTCP2).
Ujenzi wa awamu ya kwanza ya mradi huo wa BRT ulikamilika mwaka 2015 na unahusisha barabara ya urefu wa kilometa 21, yenye vituo vikubwa vitano, vituo 27, vituo vitatu vya matoleo, vituo vitatu vya kuunganisha na mfumo wa sasa wa usafiri wa umma jijini, pamoja na sehemu mbili za maegesho ya magari.
Mradi huo ulianza mwaka jana baada ya kuwasili kwa mabasi ambayo yanaendeshwa na Kampuni ya Usafiri Jijini Dar es Salaam (UDART).
chanzo;habarileo.
Comments