Amesema serikali iko katika hatua za mwisho za mazungumzo na
mwekezaji, kabla ya kuanza uzalishaji kwenye miradi ya makaa ya mawe ya
Mchuchuma na chuma cha Liganga.
Miradi hiyo inatekelezwa kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania
kupitia Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) na Kampuni ya Sichuan Hongda
(Group) Ltd (SHG) ya China.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na wananchi wa
Kata ya Mundindi wilayani Ludewa mkoani Njombe, baada ya kukagua eneo la
mradi wa chuma cha Liganga.
Kwa mujibu wa taarifa ya ofisi ya Waziri Mkuu, Majaliwa alisema,
“Madini haya yana viwango vya juu vya ubora, hivyo ni lazima tuwe makini
kabla ya kuanza kwa uzalishaji wake. Kwani chuma chetu ni bora na
tutachimba kwa zaidi ya miaka 50.
“Hivyo maeneo haya ni nyeti na lazima
serikali ijipange vizuri na kujiridhisha, kama vipengele vyote vya
mkataba vimetengamaa ndipo mradi huo uanze.”
Hata hivyo, alisema mradi huo hautachukua muda mrefu utaanza, hivyo wananchi wawe na subira.
“Hatutaki kusikia tena suala la mikataba mibovu, tunataka mikataba itakayoleta tija,” alieleza.
Akizungumzia fidia kwa wananchi wanaopisha mradi, alisema kabla
haujaanza, lazima walipwe fidia zao na tayari fedha zipo mwekezaji
anasubiri ruhusa ya serikali.
Alisema kuna baadhi ya watu wamejipenyeza na kutaka kuiibia serikali kupitia suala la ulipaji wa fidia.
Alisema Serikali haiko tayari kuona wananchi hao, wakitumika kama
madaraja ya wizi. Alisema watu hao ambao hawahusiki na eneo hilo,
wamesababisha gharama za fidia kuwa kubwa, hivyo wataalamu wanatathmini
ili kubaini wahusika kabla ya kulipa.
“Tunataka wananchi wenyewe waliokuwa hapa ndiyo tuwalipe fidia yao
kwa mujibu wa tathmini husika. Fidia yenu mtalipwa baada ya kuwaondoa
wezi wote waliojipenyeza. “Kuna watu wanataka kuiibia serikali kwa
mgongo wenu, hili hatutakubaliana nalo. Tupo makini, vumilieni, serikali
inalifanyia kazi suala letu. Hakuna haki ya mtu itakayopotea,” alisema.
Naibu Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Tanzania China International
Mineral Resources Ltd (TCIMRL), Eric Mwingira alisema miradi ya Liganga
na Mchuchuma, inatekelezwa kwa mfumo unganishi ambayo ina vipengele
vitano kikiwemo cha mgodi wa chuma cha Liganga.
Alisema mgodi huo wa chuma una uwezo wa kuzalisha tani milioni 2.9
kwa mwaka huku kiwanda cha kuzalisha bidhaa za chuma Liganga kitazalisha
tani milioni 1.1 kwa mwaka.
Mwingira alisema kipengele kingine ni mgodi
wa makaa ya mawe Mchuchuma wenye uwezo wa kuzalisha tani milioni tatu
kwa mwaka.
“Kipengele cha nne ni kituo cha kufua umeme cha megawati 600 huko
Mchuchuma. Kati ya hizo megawati 250 zitatumika Liganga katika kuchenjua
na kuzalisha chuma cha pua na megawati nyingine 350 zitaingizwa kwenye
msongo wa Taifa ili kuiuzia Tanesco,” alisema.
Pia kutakuwa na njia ya msongo wa umeme wa kilowati 220 kati ya
Mchuchuma na Liganga na barabara ya mkato kutoka Mchuchuma hadi Liganga.
Alisema gharama za uwekezaji katika mradi huo unganishi ni dola la
Marekani bilioni tatu, ambapo dola milioni 600 ni mtaji wa mwekezaji na
mkopo utakuwa dola bilioni 2.4.
Awali, Mbunge wa Ludewa, Deo Ngalawa alimuomba Waziri Mkuu kuwaeleza
wananchi hao ni lini watalipwa fidia za kupisha mradi wa chuma Liganga
na mradi huo utaanza lini.
chanzohabarileo.
Comments