Viongozi wa mkoa wa Tanga na Manyara wametakiwa kusimamia kikamilifu
utaratibu huo na kuhakikisha kila mwananchi mwenye silaha katika wilaya
hizo katika mikoa yao awe anamiliki kihalali ama la, anaripoti kituo cha
polisi ili zikaguliwe upya.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana katika ziara yake ya siku moja ya
kutembelea katika eneo la mgogoro wa mpaka uliodumu kwa muda mrefu kati
ya wilaya ya Kilindi na Kiteto, eneo la Lembapuli ambapo alijionea eneo
lililofyekwa mpaka upya wa ziada wa kilometa 2.5 kila upande wa wilaya
hizo zilizokuwa zikidaiwa na kugombaniwa na wananchi wa pande zote
mbili.
Alisema wakuu hao wa mikoa wanatakiwa kufanya msako wa nyumba kwa
nyumba ili kubaini watu wenye silaha na kuhakikisha silaha zote
zinapelekwa kituo cha polisi ili zihakikiwe upya na kwamba baada ya
hatua hiyo, adhabu kali zitachukuliwa kwa wananchi watakaokaidi agizo
hilo.
“Nimepata habari za watu wanamiliki silaha kiholela, nawaagiza wakuu
wa mikoa kuanzia leo (Januari 18) natoa wiki moja kila mwenye silaha
akaripoti kituo cha polisi ili ikaguliwe upya kwa kushirikiana na kamati
zenu za ulinzi na usalama, ”alisema.
Alikemea tabia ya kuwakamata watu hovyo iliyokuwa ikiendelea katika
mgogoro huo wa mpaka na kuwataka kuacha mara moja kwa kuwa wananchi hao
ni ndugu na ni watanzania wana uhuru wa kufanya shughuli zao sehemu
yeyote ili mradi wanafuata sheria, taratibu za maeneo husika na nchi kwa
kuwashirikisha viongozi wao.
Sambamba na hilo alisisitiza kuwa mpaka utakaotenganisha wilaya hizo
ni mpaka wa kiutawala uliowekwa kwa GN 65 mwaka 1961 na kwamba amefuta
mpaka wa kilometa 2.5 uliowekwa kiholela na wilaya za Kilindi na Kiteto
ambao ndio chimbuko la mgogoro huo.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dk Joel Bendera alipongeza uamuzi wa
waziri mkuu wa kuhakikisha mauaji yanakomeshwa, uporaji wa mali na
uharibifu wa nyumba na vitendo vingine ambapo amerejesha hali ya amani
na utulivu katika maeneo hayo iliyotoweka kwa miaka mingi.
Kwa miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na alama na Gn nyingine
zilizozaliwa kila upande wa wilaya hizo ambazo ndizo zimeleta mgogoro
huo baada ya kuzaliwa wilaya ya Kilindi na wilaya ya Kiteto, ambapo
awali ilikuwa wilaya moja iliyojulikana kama Masai District ikiwa na
wilaya ya Monduli na Simanjiro na baadaye kugawanyisha wilaya hizo.
CHANZO;HABARILEO.
Comments