Majaliwa aliyekuwa mkoani Katavi kwa ziara maalumu alitoa agizo hilo
muda mfupi kabla hajafungua rasmi duka la dawa lililojengwa katika
Hospitali ya Manispaa ya Mpanda huku akiuliza “kwa nini Mtwara?”
Alisema lazima zipo sababu za mkoa huo kufanya vibaya katika matokeo
ya mtihani huo hivyo kuna ulazima wa wizara hizo mbili kwenda mkoani
humo kufanya uchunguzi wa kina ili kuzibaini sababu hizo.
“Haiwezekani kwa shule kumi nchini zilizoshika mkia kati ya hizo
shule tisa zikitoka katika mkoa mmoja lazima kuna sababu ...naziagiza
Wizara ya Elimu na Ufundi Stadi na Tamisemi kwenda mkoani Mtwara na
kufanya uchunguzi wa kina ili ziweze kujua kuna nini ….kwa nini Mtwara,”
alihoji Waziri Mkuu.
Aliupongeza Mkoa wa Katavi kwa kushika nafasi ya pili kitaifa baada
ya Mkoa wa Geita kwa kufanya vizuri katika matokeo ya Taifa wa kumaliza
Elimu ya Msingi mwaka 2016 huku akiziagiza halmashauri nchini kupitia
idara ya ukaguzi kuhakikisha shule na walimu wanakaguliwa mara kwa mara
ili kuongeza ubora utoaji wa elimu.
Awali, akisoma taarifa ya mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Raphael
Muhuga alimweleza Waziri Mkuu kuwa kwa miaka kadhaa mkoa huo umekuwa
ukishika nafasi ya kwanza nchini katika matokeo ya mtihani wa kitaifa wa
kuhitimu Elimu ya Msingi nchini, na kwamba wamejipanga kuhakikisha
mwaka huu wanarejea kileleni.
chanzo;habarileo.
Comments