Aidha, Mchungaji wa Kanisa la Bonde la Baraka, ameingizwa lawamani kwa kupotosha umma.
Haruna aliyekuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kifafa tangu udogo wake,
alikutwa na wazazi wake Jailo Kyando (36) ambaye ni muosha magari na
mkewe, Anna Elieza (32) akiwa amefia usingizini Jumatatu wiki hii
nyumbani kwao Mtaa wa Igoma A, Kata ya Isanga jijini hapa.
Kilichowapa taharuki wakazi wengi jijini hapa ni baada ya ndugu,
jamaa na marafiki wa familia ya Haruna walipotoka makaburini siku hiyo
walikokwenda kuzika, waliporejea nyumbani waliukuta mwili wa mtoto huyo
ukiwa umelazwa kwenye godoro, pale pale ulipowekwa wakati walipokuwa
wakiuandaa kuuweka kwenye jeneza.
Hatua hiyo ilizua taharuki kubwa kiasi cha wananchi kutaka kufahamu
ni kitu gani kilichozikwa ndani ya jeneza na ndipo Jeshi la Polisi
lilipoingilia kati, kuzuia kufukuliwa kwa kaburi husika.
Hatua hiyo ilisababisha vurugu na hatimaye saa tatu za usiku siku
hiyo hiyo ya maziko ya awali, Polisi wakalazimika kutumia mabomu ya
machozi, kutawanya watu waliofurika katika makaburi ya Isanga
wakishinikiza kaburi lifukuliwe.
Lakini juzi baada ya kukamilishwa kwa taratibu husika, ikiwemo
kupatikana kwa kibali kutoka mahakamani, saa nne na nusu asubuhi, Polisi
Mkoa wa Mbeya walifika eneo la makaburi alipozikwa marehemu na
kusimamia shughuli nzima ya kufukua kaburi hilo.
Shughuli hiyo iliyodumu kwa muda wa nusu saa kama ilivyokuwa siku ya
kwanza, ilihudhuriwa na mamia ya wakazi jijini hapa waliotaka kujua nini
kilichozikwa ilhali mwili ukiwa umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa
Kanda ya Mbeya kwa wakati huo.
Nusu saa baadaye jeneza la mtoto huyo lilitolewa nje ya kaburi na
ndipo Mwenyekiti wa Mtaa wa Igoma A, Fredy Mwaiswelo alipofunua jeneza
na kukuta ndani kukiwa tupu, hali iliyoashiria mwili wa marehemu
haukuwekwa ndani ya jeneza wakati wanakwenda kuzika.
Kutokana na hali hiyo, Polisi kwa kushirikiana na baadhi ya vijana,
walibeba jeneza hilo na kuelekea nalo katika Kituo cha Polisi kwa ajili
ya uchunguzi zaidi kabla ya kuwakabidhi tena wanandugu mwili ili
kuendelea na taratibu za maziko kwa mara nyingine.
Baada ya ndugu kukabidhiwa mwili, jeshi hilo pia lilisimamia maziko
yaliyofanyika upya saa 10 jioni katika kaburi lile lile la awali, lakini
tofauti na awali, kabla ya kuzika ulifanyika utaratibu wa ndugu, jamaa
na marafiki waliohudhuria, kuuaga mwili wa marehemu uliokuwa ndani ya
jeneza lililofunuliwa upande wa kichwani.
Kutokana na mkanganyiko uliojitokeza, baadhi ya ndugu na majirani wa
Mtaa wa Igoma, walisema tukio hilo linaweza kuwa na sura mbili kwa maana
ya hujuma iliyofanywa kwa makusudi, ikilenga maslahi binafsi ya mtu
inayohusishwa na imani za kishirikina au bahati mbaya ya kuusahau mwili
wa marehemu.
Walisema inaweza kuwa hujuma kutokana na kawaida ya misiba kabla ya
maziko, lazima ndugu watoe heshima za mwisho kwa marehemu, lakini kwa
msiba huu haikufanyika pamoja na baadhi ya ndugu kutohudhuria mazishi.
Akizungumza na gazeti hili nyumbani kwake jana pamoja na kukanusha
tuhuma za kuhusisha tukio hilo na imani za kishirikina, baba wa marehemu
alisema mkanganyiko uliojitokeza wakati taratibu za kuuandaa mwili
zikifanyika pamoja na uzushi uliofanywa na mchungaji, ambaye alisema
hamjui kwa jina, ndiyo vilivyokuza jambo hilo.
Alisema kama ilivyo kawaida baada ya majirani kupata taarifa za msiba
wakiwa nyumbani hapo, walichanga fedha na kutuma watu kwenda kununua
jeneza.
“Wananchi walichanga hela wakanunua jeneza likaletwa nyumbani.
Waliobeba jeneza walilisukumiza tu kwenye chumba wakatoka, sisi
tukaendelea na taratibu nyingine za mazishi. Baadaye akaja mwenyekiti
akasema toeni mwili wa marehemu nje, wakatoa meza nje wakatuma vijana
waende kuchukua mwili wa marehemu ndani. Waliopeleka jeneza ndani na
waliokwenda kulichukua ni watu wengine.
Jeneza likawekwa juu ya meza
tukaendelea na mahubiri,” alisema Kyando.
Alisema baadaye walikwenda kuzika na baada ya kuzika walirudi
nyumbani kisha wakala chakula na kunawa maji, kama ilivyo desturi ya
misiba mingi mkoani hapa.
“Tumenawa maji tukakaa. Baada ya kukaa kuna mgeni akaingia katika
chumba tunacholala ambapo awali ndipo tulimlaza mtoto kwenye kigodoro,
alipoweka begi akakuta kuna blanketi. Alipolifunua akashtuka akasema
kuna nyoka watu wakaanza kukimbia ndani. Baadhi ya watu wenye roho yenye
hasira wakaamua kuingia ndani wakahakikishe kuna nini,” alisimulia.
“Walipoingia ndani ndipo wakakuta ni mwili wa mtoto yaani marehemu.
Waliposema ni mtoto wakipaza sauti watu wakajaa ndani. Ndipo waumini wa
yule mchungaji wakaanza kumpigia simu yule mchungaji baadaye akarudi.”
Alisema baada ya mchungaji huyo kufika, aliingia ndani na waumini wake na kuanza kuomba.
“Walipoomba kwa muda mrefu ndipo mchungaji huyo alipotoka nje na
kushika MIC na kuuambia umati kuwa mtoto baada ya kuombewa amehema mara
mbili na ndipo watu wakaanza kulumbana,” alieleza.
“Kama siyo mchungaji kuzusha yale wala yasingekuzwa mpaka kwenye
mitandao kiasi hiki. Sisi tunaamini walioagizwa kuchukua mwili
walichukua jeneza tupu pasipo kuwekwa mwili ndani yake na kwa kuwa baada
ya kutolewa jeneza hatukuingia ndani hivyo tuliuacha mwili nyumbani
tukaenda kuzika jeneza peke yake,” alibainisha.
Akizungumzia suala la imani ya familia hiyo, Kyando alisema awali
yeye na familia yake yenye watoto wawili, walikuwa wakisali katika
Kanisa Katoliki, lakini kutokana na matatizo ya degedege yaliyokuwa
yakimsumbua mwanawe wa kwanza, mkewe aliamua kumpeleka mtoto huyo kwa
mchungaji wa Kanisa la Bonde la Baraka ili aombewe ikiwa ni sehemu ya
kuhangaikia afya ya mtoto.
“Tulikuwa tunasali Roma, lakini kutokana na matatizo ya mtoto, mama
yake akaamua aanze kusali Kanisa la Bonde la Baraka ili aombewe.
Hapo
mimi nikaacha kusali na ndiyo sababu hata katika ibada ya maziko ya
mtoto ikabidi tulishirikishe kanisa walikokuwa wanasali mama na mtoto,”
alisema Kyando na kuongeza:
“Watu wamezungumza maneno mengi sana, siwezi
kubisha japo ni ya uzushi ila wameongea kutokana na walivyosikia, ila
ukweli naujua mimi na namwachia Mungu.”
Naye baba mkubwa wa marehemu, Saulo Kyando alisema jambo lililotokea
lilikuwa la kawaida na kilichotokea ni kukosekana kwa uratibu makini wa
msiba huo.
“Hili jambo lilikuwa la kawaida sema kilichokosekana ni mtu ambaye
angeliweka jambo sawa, angekuwepo mtu wa kusimamia kila hatua
yasingefikia hapa,” alisema Saulo.
chanzo;habarileo.
Comments