Pia Rais amewataka wananchi pamoja na kulima mazao yanayohimili ukame, wahifadhi chakula kwa faida ya baadae pale mabadiliko ya hali ya hewa yanapotokea wasipate shida.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kwa niaba ya Rais Magufuli baada ya kusimikwa rasmi Askofu Dk Elias Nassari kuwa Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Dayosisi ya Meru jana, shughuli iliyofanyika katika Mji wa Usa wilayani Arumeru mkoani Arusha.
Dk Magufuli alisema kuwa kwa sasa serikali iliyopo madarakani ni ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) na imepanga mipango yake ya maendeleo kwa mujibu ya ilani ya chama chake na inataka kuitekeleza kama ilivyoahidi katika uchaguzi uliopita.
“Tunataka viongozi wa dini kuwahubiria waumini wao katika makanisa na misikitini juu ya hilo ili kila mmoja afanye kazi na sio sasa kwani serikali ina mipango mingi ya kutaka mwananchi wa kawaida hasa mnyonge kunufaika na matunda ya nchi yake,” alisema.
‘’Tukianza kuzungumza huku na kule katika majukwaa tutakuwa tunawachanganya wananchi, kikubwa ni kukubali aliyepo madarakani kumpa nafasi atekeleze aliyoahidi na kusubiri muda nawe utakuwa na la kusema lakini sio sasa,’’ alisema Rais.
Akizungumzia ukame, Rais alisema kuwa ni jukumu la viongozi wa dini pia kuelimisha wananchi kuwa mabadiliko ya tabia ya nchini ndio yaliyofanya hali hiyo ijitokeze hapa nchi na wananchi wanapaswa kulima mazao ya kuhimili ukame na sio vinginevyo.
Rais alisema mbali ya kuhimili ukame kwa kulima mazao yenye kuhimili ukame pia wakulima na wananchi wengine wametakiwa kuhifadhi na kutunza chakula kwa faida ya baadae.
Alisema hali iliyopo ya mabadiliko ya tabia ya nchi haikuletwa na serikali bali ni mabadiliko ya hali ya hewa hivyo sote tunapaswa kujipanga kwa hali hiyo na viongozi wa dini nao wana jukumu kubwa la kuwaelimisha wananchi kulima mazao ya ukame na kuhifadhi chakula na sio kuiachia serikali pekee yake.
Kuhusu amani, Rais Magufuli alisema si jukumu la serikali pekee yake kuhubiri amani bali ni jukumu la kila mtanzania, hususani viongozi wa dini kuhubiri amani kanisani na misikitini na kupingana na wale wenye nia mbaya ya kutaka kuleta machafuko hapa nchini.
Alisema amani ikivurugika haiwezi kuchagua mtu bali ikawakumba watu wote bila ya kujali ni kiongozi wa dini, mwanasiasa ama mtu baki kwani jukumu la viongozi wa dini ni kuhakikisha mnahubiri amani nyakati zote bila ya kuchoka kwa maslahi ya watanzania wote.
Akizungumzia migogoro ya ardhi ambayo kwa kiasi kikubwa iko katika wilaya ya Arumeru alisema na kuwataka viongozi wa dini tena ardhi katika wilaya hiyo ni ndogo na wananchi ni wengi, lakini walionayo wanapaswa kuheshimiwa wakati serikali ikijipanga kuangalia namna ya kutatua migogoro hiyo.
Alisema na kulisifu kanisa la KKKT nchini kwa jinsi linavyojitoa katika kujenga shule na miundombinu mingine na kuwataka kuendelea na hali hiyo kwa kasi ya hali ya juu na sio vinginevyo.
Mkuu wa KKKT nchini, Dk Fredrick Shoo aliomba serikali kufanya tathimini ya uhaba wa chakula kote nchini ili iwe na majibu sahihi ya hali iliyopo. Dk Shoo alisema kuwa kuna baadhi ya mikoa kuna hali mbaya sana ya ukame na inatishia uhaba wa chakula na kinachotakiwa kufanywa na serikali kufanya tathimini ya kina na kuja na majibu sahihi na nini cha kufanya kutokana na tathimini hiyo.
Alisema kuna baadhi ya familia ziko katika hali mbaya za uhaba wa chakula na hilo halina kificho ila kinachotakiwa kwa serikali kufanya tathimini ili iwe na majibu sahihi ni familia ngapi ziko katika hali hiyo ili hatua madhubuti ziweze kuchukuliwa.
“Serikali isifanye mzaha katika jambo hili kwani tutakuwa tunamkosea mungu na kwa wananchi kwa ujumla na ni jukumu la serikali na kufanya tathimini ya hali hiyo ili kuchukua hatua stahiki,’’ alisema
Akizungumza baada ya kusimikwa kuwa Askofu wa Dayosisi ya Meru, Askofu Dk Nassari alisema dawa kubwa ya yeye kuiongoza Dayosisi hiyo ni kuungana kwa makundi yote kuwa kitu kimoja, kwani kazi yake itakuwa rahisi kwa maslahi ya wana Meru.
Askofu Nassari alisema mzigo aliotwishwa nao nimzito lakini kama waumini wote watamtanguliza Mungu na kufanya kazi kwa upendo na huruma hakika mzigo huo unakuwa mwepesi kwake.
Sherehe hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na vyama vya siasa akiwemo Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinga, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Lekule Lazier, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari na Mbunge wa Iramba, Lazaro Nyarandu.
chanzo;habarileo.
Comments