
Madiwani hao kutoka kamati za Elimu, Afya, Maji na Uchumi, Ujenzi na
Mazingira wamegoma kupokea posho ya Sh 40,000 kwa kila kikao wakitaka
kulipwa posho ya awali ya Sh 82,000.
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, John amekiri kususiwa posho
hizo na kuongeza kuwa hatua hiyo inafuatia kufuatwa kwa waraka wa
serikali wa mwaka 2007 na 2012 unaoelekeza viwango stahili vya posho kwa
madiwani.
Mkurugenzi amesema waraka huo wenye Kumb Na CHB/443/01 wa Novemba 26,
2007 umetaja viwango vya malipo ya madiwani kwa mwezi, posho ya
madaraka kwa wenyeviti wa kamati, wenyeviti wa halmashauri za wilaya,
manispaa na majiji nchini na kwamba yeye ni msimamizi na hafanyi kwa
matakwa yake.
Amesema, kutumika kwa waraka huo kutaisaidia halmashauri kuokoa zaidi
ya Sh milioni 60 ambazo zitatumika katika miradi ya maendeleo kama
afya, elimu na maji.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Evarist Silayo amesisitiza msimamo
wake kwamba posho ya kikao ni Sh 82,000 kama ilivyo kwa halmashauri
nyingine mkoani Kilimanjaro ambazo zipo juu ikilinganishwa na Rombo.
“Posho hii tumeikuta ilipitishwa na madiwani wa awamu zilizotangulia
lakini pamoja na hilo tulipoingia sisi tulijaribu kuondoa vyakula wakati
wa vikao vya kamati... hakuna diwani wa Rombo analipwa posho ya
usafiri, madaraka isipokuwa wenyeviti wa kamati na mwenyekiti wa
halmashauri,” amesema.
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Rombo linaundwa na
madiwani 38, wakiwamo 28 wa kata, huku kati yao 37 ni kutoka Chadema na
mmoja kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM).
chanzo;habarileo.
Comments