Lowassa alisema hayo katika kampeni za kumnadi mgombea udiwani wa
kata hiyo. Alisema kilichofanywa na vyama vya upinzani ni kugawa kura,
wakati upinzani ulikuwa na nafasi kubwa ya kushinda.
Alisema vyama vinavyounda Ukawa vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi,
kila kimoja kimesimamisha mgombea udiwani katika kata hiyo, kwa hali
hiyo uwezekano wa kushinda ni mdogo sana, hivyo kukipa mwanya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) kushinda kiti hicho.
Akizungumza katika kampeni za Chadema zilizofanyika katika Kitongoji
cha Ematasia, Lowassa alisema vyama hivyo tayari vimeshafanya kosa la
kiufundi, linaloweza kusababisha vyama hivyo ‘kuangukia pua’ katika
uchaguzi huo na kuiwezesha CCM kuibuka na ushindi asubuhi na mapema.
Alisema CCM ina nafasi kubwa ya kushinda katika uchaguzi huo,
kutokana na kuwa na uhakika wa kura zake, kutokana na kutokuwa na
upinzani wa chama kingine chenye mrengo wake, kama ilivyo kwa vyama
hivyo vya Ukawa, ambavyo viko katika hatari ya kugawa kura.
“Nyie tayari mmeshafanya makosa makubwa ya kiufundi kwa kila chama
cha Ukawa kusimamisha mgombea wake, hapo ndipo CCM wanaposhindia, kwa
hiyo mwendelee mkijua mna kazi kubwa kushinda,” alisema Lowassa.
Katika hali ya kushangaza Lowassa alijikuta akimuombea kura mgombea
wa CCM, Julius Savoyo aliposema wananchi wa kata hiyo wanapaswa kumpa
kura na kumuweka madarakani mgombea aliyeshinda katika uchaguzi uliopita
wa mwaka 2015, pasipo kujua diwani aliyeshinda wakati huo na
kutenguliwa na mahakama ni wa CCM.
“Wananchi wa kata hii hamna kazi ngumu katika uchaguzi pamoja na
makosa yaliyofanywa na vyama vya Ukawa, hakikisheni mnamrejeshea udiwani
yule aliyeshinda wakati ule ili aendelee na kazi yake,” alisema
Lowassa.
Akizungumza katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni za CCM, Katibu wa
Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Shaaban Mdoe alisema kitendo
kilichoonekana na Lowassa kuwa ni kosa kusimamisha wagombea wa vyama vya
Ukawa ni utabiri mzuri wa ushindi kwa CCM, kama alivyosema tena katika
kampeni za uchaguzi wa Urais mwaka juzi.
Hata hivyo, Mdoe alisema suala la Ukawa kwa sasa halipo tena, bali ni
Ukiwa na ndiyo maana kila chama cha muungano huo, kinajaribu bahati
yake kutokana na kuvunjika kwa ndoa hiyo ; na wa mwisho kuondoka katika
ndoa hiyo, alikuwa ni Mwenyekiti wa Taifa wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia.
Mdoe alisema kitendo cha Lowassa kumnadi mgombea wa CCM, si bahati
mbaya bali ni ukweli uliopo ndani ya moyo wake, kwa kuwa hata
akijifungia chumbani kwake peke yake, anakubali kazi nzuri inayofanywa
na serikali ya Rais John Magufuli.
chanzo; zanzibar24.
Comments