Kilimanjaro haina upungufu wa chakula; ina akiba ya kutosha.

SERIKALI mkoani Kilimanjaro, imesema haina upungufu wa chakula. Hata hivyo, imepiga marufuku wananchi na wafanyabiashara kutengeneza pombe kwa kutumia nafaka kwani kufanya hivyo itapunguza akiba ya chakula iliyopo mkoani humo.

Katika msimu wa kilimo wa mwaka 2015/2016 mkoa huo ulikadiria kuzalisha tani milioni 1.8 za chakula huku kiasi kilichozalishwa kikiwa tani milioni 1.3 za mazao ya chakula yakijumuisha mazao ya nafaka, mizizi, ndizi na mikunde ambao ni sawa na asilimia 73 ya lengo.

Mkuu wa Mkoa huo, Saidi Mecky Sadiki alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya chakula mkoani humo na mipango ya serikali katika kulinda akiba iliyopo na kushauri wananchi jinsi ya kutumia rasilimali walizonazo kujiongezea akiba ya chakula.

Alisema upungufu unaoonekana wa asilimia 27 kati ya lengo la uzalishaji chakula kwa msimu wa kilimo 2015/2016 haujaathiri akiba ya chakula iliyotarajiwa. Alisema hata hivyo akiba hiyo haijafanya mkoa kubweteka na badala yake wananchi wanahimizwa kutunza chakula walicho nacho.

“Nimetoa maelekezo kwa wakuu wa wilaya zote na wakurugenzi wa halmashauri kwamba, hakuna kutoa leseni za biashara za pombe zinazotengenezwa kwa nafaka….hili limelenga kulinda akiba tuliyonayo, pia wananchi wauze mifugo kununua chakula,” alisema Sadiki.

Alisema kati ya tani milioni 1.3 zilizozalishwa, tani 369,122 ni nafaka, 98,301 ni za mazao ya mizizi, 810,140 ni ndizi na tani 58,125 ni mazao ya mikunde.

Alisema wamefikia kiwango hicho cha asilimia 73 kutokana na mvua kunyesha kwa kiwango cha kuridhisha. Sadiki alisema kwa mwaka 2016 mkoa huo una idadi ya watu 1,739,084 ambao mahitaji ya chakula kwa watu hao ni tani 476,074 za wanga (nafaka) na 47,606 za kunde.

Hata hivyo, mkuu wa mkoa aliwataka wakazi wa mkoa huo kubadilika kulingana na wakati na badala yake kutumia zao la Ndizi kama chakula, kutolima mazao yasiyoendana na hali ya hewa, kuuza mifugo ili kununua chakula na kutouza chakula chote bila kuweka akiba.

chanzo; zanzibar24

Comments