Kabla ya kutengua uteuzi wa Mramba, Rais Magufuli ambaye Jumapili hii
alisali mjini Bukoba katika kanisa la Bikira Maria, Mama mwenye Huruma
la mjini Bukoba, alisema Tanesco haikumshirikisha yeye, Makamu wa Rais,
Waziri Mkuu na Waziri mwenye dhamana ya masuala ya Nishati na Madini,
Profesa Sospeter Muhongo.
Ewura juzi ilitangaza kupandisha bei ya umeme kwa asilimia 8.5 baada
ya Tanesco kuomba gharama zipande kwa asilimia 18.19, lakini hatua hiyo
ilisitishwa na Profesa Muhongo.
“Waliopandisha umeme hawakuja kuniuliza hata mimi kiongozi wa nchi,
hawakuuliza hata waziri mwenye dhamana, ya nishati hawakumuuliza hata
Makamu wa Rais, Waziri Mkuu haiwezekani mtu akae pekee yake na afanye
maamuzi yake pekee bila kushirikisha mamlaka nyingine,” alisema Rais.
Uteua bosi mpya, taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya
Rais, IKULU, Gerson Msigwa ilieleza kuwa Rais Magufuli baada ya kutengua
uteuzi wa Mramba, amemteua Dk Tito Mwinuka kuwa Kaimu Mkurugenzi
Mtendaji wa Tanesco.
Mwinuka ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM) na hadi
uteuzi wa jana, alikuwa ni Mkuu wa Idara ya Mekanika na Uhandisi wa
Viwanda Chuo cha Uhandisi na Teknolojia (CoET) cha Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam.
Akiwa kanisani, Rais Magufuli alimpongeza Profesa Muhongo kwa hatua
ya kusimamisha kupanda kwa bei ya umeme. “Namshukuru waziri wa nishati
kwamba ameshatengua maamuzi hayo, kwa hiyo umeme hakuna kupanda”.
Rais Magufuli alisema haiwezekani watu mnapanga mikakati ya kujenga
viwanda na hasa katika mikakati hii mikubwa ya nchi ya kusambaza umeme
hadi vijijini na umeme huo unaenda hadi kwa watu maskini walioumbwa kwa
mfano wa Mungu, halafu mtu pekee kwa sababu ya cheo chake anakwenda
kusimama kupandisha bei ya umeme.
Akionekana kukereka kwa hatua hiyo ya kupandishwa kwa bei ya umeme,
Rais Magufuli alisema, “Na ndio maana baba askofu nalizungumza hili
kwamba majipu bado yapo na nitaendelea kuyatumbua, ndio maana naomba
sana Watanzania muendelee kutuombea, lengo la serikali ninayoiongoza ni
kwenda na wananchi wa kipato cha chini.”
chanzo; zanzibar24.
Comments