Uteuzi wa Kilango unazidi kuongeza joto kuwa huenda kukafanyika
mabadiliko katika Baraza la Mawaziri, ukizingatia uteuzi uliofanywa na
Dk Magufuli wiki iliyopita wa kumteua aliyekuwa Naibu Waziri, Ofisi ya
Waziri Mkuu (Wenye Ulemavu), Dk Abdallah Possi kuwa Balozi; pamoja na
uteuzi wa wabunge wengine wawili.
Kabla ya Anne Kilango, Dk Magufuli pia alifanya uteuzi wa wabunge
wengine wawili, Profesa Palamagamba Kabudi na Abdallah Bulembo kuwa
wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika nafasi zake
10 alizonazo kwa mujibu wa Katiba.
Juzi usiku, Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu ilitangaza kuwa
Rais Magufuli amemteua Anne Kilango Malecela kuwa Mbunge wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kwamba ataapishwa kwa mujibu wa
taratibu za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kilango alisema anamshukuru Mungu
pamoja na Rais Magufuli kwa kuwa na imani naye na kuamua kumteua tena
katika nafasi hiyo.
“Kwa kweli sina maneno mengi, namshukuru Mungu na pia ninamshukuru
Rais wangu kwa kuwa na imani tena kwangu na kuamua kunipa nafasi hii.
Nimekuwa mbunge kwa miaka 15, ni kazi ninayoielewa na ninamuomba
Mwenyezi Mungu aniwezeshe ili nifanye kazi itakayowaridhisha,” alisema
mbunge huyo wa zamani wa Same Mashariki mkoani Kilimanjaro, ambako
alihudumu kwa miaka 15 hadi aliposhindwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka
2015.
Mbunge huyo mteule alisema pia anakwenda bungeni kwa ajili ya
serikali, wananchi pamoja na kwenda kukitetea chama chake (Chama Cha
Mapinduzi) pamoja na kurekebisha pale panapostahili, lengo likiwa ni
kuunga mkono Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dk Magufuli.
“Mungu ana sababu ya kunirejesha tena bungeni. Nitakwenda kufanya
kazi nitakitetea chama changu na kukikosoa pale panapostahili pamoja na
kuwatetea wananchi wangu na serikali kwa ujumla,” alifafanua Kilango
ambaye katika Bunge la Tisa, alijipambanua kuwa mmoja wa wabunge mahiri
na kujikita katika kupambana na ufisadi.
Baada ya kushindwa Uchaguzi Mkuu kwa mgombea wa Chadema, mapema mwaka
jana, Dk Magufuli alimteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, lakini
alidumu katika nafasi hiyo kwa muda wa mwezi mmoja tu, baada ya Rais
kutengua uteuzi wake Aprili 11, mwaka jana.
Alitenguliwa nafasi hiyo baada ya kutangaza kwenye vyombo vya habari
kuwa mkoa wake hauna watumishi hewa, jambo ambalo lilisababisha Ikulu
kufanya uchunguzi wake na kubaini kuwepo kwa watumishi hao, hivyo yeye
na Katibu Tawala wake, Abdul Rashid Dachi wakaondolewa katika nyadhifa
zao.
“Na wale wote wa Shinyanga ambao walisemekana ni zero, hakuna
mtumishi hewa, walikuwa tayari wameshalipwa shilingi milioni 339.9,
nimejiuliza sana, na nikajiuliza sana na kwa kweli nimejiuliza sana na
kwa masikitiko makubwa, kwa nini Mkuu wa Mkoa alisema hakuna mtumishi
hewa?” alisema Dk Magufuli wakati akitangaza kuwavua madaraka Kilango na
Dachi.
Kilango ambaye ni mwanamke mpambanaji, mwishoni mwa utawala wa
Serikali ya Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete aliteuliwa kuwa Naibu
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, wadhifa alioushikilia hadi
wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Uteuzi wake huo pamoja na wa kina Profesa Kabudi na Bulembo, sanjari
na kubadilishiwa kazi kwa Dk Possi, kunazidi kuongeza joto la mabadiliko
katika Baraza la Mawaziri, kwani hadi sasa, katika wateule wote wa
ubunge wa Dk Magufuli, wamepewa uwaziri ukiondoa mmoja, Naibu Spika Dk
Tulia Ackson.
Wabunge wa Kuteuliwa na Dk Magufuli ambao baadaye aliwateua kuwa
mawaziri ni Profesa Makame Mnyaa Mbarawa (Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano), Balozi Dk Augustine Mahiga (Mambo ya Nje ya Ushirikiano wa
Afrika Mashariki), Dk Philip Mpango (Fedha na Mipango), Profesa Joyce
Ndalichako (Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi) na Dk Possi
ambaye sasa amemteua kuwa Balozi.
Kwa uteuzi wa Kilango, Rais Magufuli amefikisha idadi ya wabunge
wanane wa kuteuliwa na amebakiza nafasi mbili kwa mujibu wa Katiba. Anne
Kilango ni nani?.
Alikuwa Mbunge wa Same Mashariki kwa miaka kumi kuanzia 2005 hadi
2015 na alikuwa Mbunge wa Kuteuliwa na Rais kwa miaka mitano kuanzia
mwaka 2000 hadi 2005.
Alihitimu Diploma ya Ualimu katika Chuo cha Ualimu Chang’ombe, Dar es
Salaam na Cheti cha Utawala Bora kutoka Chuo Kikuu Makette, Wisconsin
nchini Marekani. Alipata Digrii ya Masuala ya Biashara kutoka Chuo Kikuu
Huria cha Tanzania (OUT)na ana Digrii ya Pili ya Elimu ya Biashara
kutoka ESAMI, Arusha.
Anne alihitimu elimu ya msingi katika shule ya Jitengeni mkoani
Kilimanjaro na kidato cha nne alihitimu Shule ya Sekondari Weruweru
mkoani Kilimanjaro. Alihitimu kidato cha sita katika Shule ya Sekondari
ya Shycom mkoani Shinyanga.
Amewahi kuwa mjasiriamali, Mhasibu Mkuu wa Shirika la Ndege la KLM,
Mdhibiti wa Fedha wa Shirika la Ndege la Gulf Air, Mhasibu Msaidizi wa
Shirika la Ndege la ATC na Mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana
Kisutu jijini Dar es Salaam. Pia amewahi kuwa Mwenyekiti wa UWT wa
Wilaya ya Kinondoni, mkoani Dar es Salaam.
chanzo;habarileo.
Comments