Kikundi cha ushirika Nguvu Kazi pemba chapokea msaada.



Image result for pemba islandNa Asha Salum.

IDARA ya Maendeleo ya Uvuvi Kisiwani Pemba, imekabidhi majembe matano (5), Mapauro kumi na tano (15), na shoka mbili (2),vikiwa na thamani ya shilingi laki mbili na elfu sita (26000/=), kwa Wanaushirika wa kikundi cha Ufugaji Samaki kinachojulikana kwa jina la ‘Nguvu Kazi’ ,kilichopo Chamabani, Wilaya ya Mkoani.

Akikabidhi kwa niaba ya Waziri wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Ofisa Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi, Sharif Muhammed Faki, amesema kuwa, vifaa hivyo vimetolewa kufuatia ahadi iliowekwa na waziri wa wizara hiyo katika ziara zake za kikazi za kawaida.

Katika maelezo yake amewataka wanavikundi hao kuzidisha bidii katika shughuli zao, kwa kuona kuwa nguvu zao zinazaa matunda na fursa ya kupatiwa vifaa hivyo kama walivyokusudia.

Pamoja na hayo, amewasihi kuvitumia vifaa walivyopatiwa katika shughuli za ufugaji wa Samaki na si vyenginevyo, ili kuongeza uzalishaji kwa faida yao na Serikali kwa ujumla.

Hata hivyo, amewasisitiza uwekaji wa kumbukumbu kwa kikundi hicho, ili kudhibiti taarifa sahihi za utekelezaji wa shughuli zao, ambazo zitatambulika na kila mmoja wa ushirika  na hata kwa viongozi wanapozihitaji .

Kwa upande wake, Ofisa Ufugaji wa Viumbe vya Baharini Pemba, Mohammed Salim Othman, alisema kuwa Serikali inajitahidi kuwapitia wananchi wake kwa ajili ya kuona maendeleo ya shughuli zao, pamoja matatizo yanayowakwamisha, ili waweze kujua ni jinsi gani ya kuwasaidia kila hali inaporuhusu.

Wakati huohuo wanaushirika wa kikundi hicho, walitoa shukurani zao kwa Waziri kwa kutekeleza ahadi alioiweka kupitia Idara hiyo, kwa kuona umuhimu wa shughuli zao kwa kuwapatia vifaa muhimu katika utekelezaji wa shughuli zao.

Nae Katibu wa kikundi hicho, Said Abrahman  Juma, kwa niaba ya wanaushirika wenzake ameahidi kuvitumia vifaa hivyo katika malengo yaliokusudiwa pamoja na uangalifu mkubwa katika shughuli zao na kufikia malengo waliojiwekea na hata kufikia kuwa kikundi bora katika ufugaji wa samaki kwa Mkoa.

Ushirika wa kikundi cha Ufugaji wa Samaki kinachojulikana kwa jina la ‘Nguvu Kazi’, kilichopo Chamabani, Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba, Kilianza shughuli zake Juni,21-2006, kwa wanachama 26 wakiwemo wanawake 12, na wanaume 14.

Comments