Aidha, kifaa hicho kina uwezo wa kufanya kazi kwenye mazingira yasiyo
na umeme na kwamba kitaweza kutumika katika vituo vya afya ili
kuwagundua wagonjwa hao mapema.
Hayo yalibainishwa Dar es Salaam jana na Naibu Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamis Kigwangwala wakati
wa uzinduzi wa kifaa hicho kilichotolewa na Kampuni ya Medomix.
Dk Kigwangala alisema kifaa hicho kitaboresha huduma za uchunguzi na
matibabu kwa tatizo la selimundu na kuongeza uelewa kwa jamii juu ya
tatizo hilo. Alisema kifaa hicho kinaweza kugundua aina mbalimbali za
selimundu kwa wagonjwa kwa teknolojia rahisi isiyohitaji matumizi ya
umeme wala wataalamu waliobobea.
“Kampuni hii imeanza kupanua huduma zake kwa kuagiza vifaa na
vitendanishi vya kutosha ili vitumike nchini. Mategemeo yangu kifaa hiki
kitatumiwa na kutoa majibu yenye ubora na hivyo kuongeza ufanisi katika
kutoa tiba sahihi kwa wagonjwa watakaogundulika,’’ alisema Dk
Kigwangala.
Alifafanua kuwa kifaa hicho kimepata usajili baada ya kupitia hatua
za usajili nchini ikiwemo kusajiliwa na bodi ya maabara binafsi za afya.
Alisema kuwa kitendo cha Kampuni ya Medomix cha kuagiza kitendanishi
cha kupima selimundu imekuja kwa wakati sahihi ambapo nchi imekuwa na
wagonjwa wengi wanaopatiwa matibabu nje ya vituo vya afya na hivyo
kufanya gharama kuwa kubwa.
“Naamini kuwa kampuni nyingine zitaunga mkono kwa kuendeleza
utaratibu huu ili huduma nyingine ziweze kutolewa kwenye vituo vya afya
wilayani na kupunguza idadi ya wagonjwa wanaopelekwa hospitali za Rufaa
za Mikoa au zile za Kanda kwa ajili ya vipimo na matibabu,’’ alieleza.
Kwa mujibu wa Dk Kigwangala, serikali imekuwa ikifanya jitihada
mbalimbali za kuhakikisha tatizo hilo linapatiwa ufumbuzi; mikakati hiyo
ni pamoja na kutengeneza mpango mkakati wa kitaifa wa kupambana na
magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo selimundu.
Pia alisema wanatoa elimu ya umma juu ya tatizo hilo, kutoa huduma za
upimaji na ugunduzi wa seli mundu, upimaji wa matatizo yanayoambatana
nayo na upimaji wa selimundu kwa watoto wachanga wanaozaliwa ili
kuwatambua mapema pamoja na kutoa huduma za tiba na kinga kutolea
huduma.
“Takwimu zinaonesha kuwa watoto wapatao 321,307 huzaliwa na tatizo la
selimundu kila mwaka. Asilimia 76 ya watoto hawa huzaliwa Afrika sawa
na watoto 237,253 kila mwaka,’’alisema na kuongeza; “Kwa hapa Tanzania
kati ya watoto 8,000 hadi 11,000 huzaliwa na tatizo hilo na kati ya
watoto hawa asilimia 15 hadi 18 ni wenye dalili za ugonjwa huo.’’
Kwa upande wake, Mratibu wa Idara ya Magonjwa ya Damu, Kitengo cha
Selimundu kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUHAS), Dk
Deogratius Soka, alisema kuwa changamoto kubwa wanazokabiliana nazo ni
uelewa mdogo wa watu kuhusu ugonjwa huo na kwamba lengo lao ni
kuwaelimisha wajitokeze kupima afya zao.
chanzo;habarileo.
Comments