Kampuni za mawasiliano zisizojisajili DSE kukiona.

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James KilabaMAMLAKA ya Mawasiliano nchini (TCRA) imesema imepanga kuzichukulia hatua za kisheria kampuni za mawasiliano, ambazo zimeshindwa kujisajili katika Soko la Hisa (DSE) kama sheria inavyoelekeza.

Hatua ya kampuni za mawasiliano kujisajili katika Soko la Hisa (DSE) ni utekelezaji wa Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA), ambayo inaelekeza makampuni yote ya mawasiliano kujisajili katika soko la hisa.

Kauli hiyo ya TCRA imekuja ikiwa ni siku chache baada ya ukomo wa kujisajili kwa kampuni hizo katika Soko la Hisa kupita ambayo ilikuwa ni Desemba 31, mwaka jana.

Akizungumza na vyombo vya habari katika Makao Makuu ya Mamlaka hiyo yaliyopo barabara ya Sam Nujoma, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kilaba alisema, hadi sasa bado hawajapokea taarifa rasmi kutoka kwa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) ya kampuni zilizojisajili na ambazo bado hazijatekeleza agizo.

Alisema baada ya kupokea taarifa kutoka CMSA, wao kama wadhibiti watatekeleza sheria hiyo ambayo inayataka makampuni ya mawasiliano kujisajili katika soko la hisa.

“Kitu cha msingi ni kwamba makampuni yote yanayotoa huduma za mawasiliano nchini yaliyotajwa kwenye sheria ile yanatakiwa kusajili, kwahiyo sisi jukumu letu ni kutekeleza sheria kwa walioshindwa au watakaoshindwa kusajili,” alisema Kilaba.

Kilaba alisema miongoni mwa adhabu ambazo zimeainishwa na sheria hiyo ni kusitisha au kufuta leseni za kampuni hizo, hivyo taarifa ya CMSA itakapowasilishwa kwa mamlaka hiyo, hatua zitachukuliwa dhidi ya kampuni zitakazokuwa hazijatekeleza agizo hilo.

Hadi sasa kampuni ni kampuni tatu pekee, ndio zimeandaa mchanganuo wake na kuwasilisha CMSA kwa ajili ya kuorodhesha kwenye soko la hisa.

Kampuni hizo ni Airtel, Tigo na Vodacom Tanzania ambazo zimewasilisha mchanganuo wake kwa CMSA kwa ajili ya kuorodhesha DSE, kama Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta inavyoelekeza.

Hapa nchini kuna kampuni saba za simu ambazo ni Airtel, Halotel, Zantel, Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Smart, Tigo na Vodacom Tanzania.

chanzo;habarileo.

Comments