UONGOZI wa Kampuni ya Uwindaji ya Orttelo Business Corporation (OBC)
inayomiliki Pori Tengefu la Loliondo, umeweka mambo hadharani mbele ya
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, ikieleza kuwa kila mwaka hutoa
msaada wa Dola za Marekani 1,037,000 (Sh bilioni 2.8) kwa Halmashauri ya
Wilaya ya Ngorongoro kwa ajili ya shughuli za maendeleo katika wilaya
hiyo.
Mkurugenzi wa OBC, Issack Mollel alisema hayo baada ya kuelezea
changamoto zinazowakuta katika utendaji kazi wa kila siku mbele ya
kamati ya wataalamu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, viongozi wa
serikali ngazi ya halmashauri, wilaya na mkoa, madiwani wa halmashauri
hiyo na viongozi wa mila na kijamii mwishoni mwa wiki.
Mollel alisema OBC haina ugomvi na jamii inayozunguka pori hususani
vijiji vinane, lakini imekuwa ikilaumiwa kila kukicha kuwa haijafanya
chochote kwa maendeleo ya vijiji hivyo wakati inatoa mamilioni ya dola
kwa ajili ya maendeleo ya afya, maji, elimu na miundombinu ya barabara
kwa kipindi chote akiwa mkurugenzi kuanzia mwaka 2006.
Alisema mbali ya kuilipa halmashauri mamilioni hayo ya dola kwa ajili
ya maendeleo ya vijiji hivyo, pia OBC huilipa Serikali Kuu mamilioni ya
dola kwa mujibu wa mkataba walionao tangu mwaka 1993.
Mkurugenzi huyo alisema baadhi ya viongozi ngazi ya wilaya, wamekuwa
wakiwachonganisha na OBC na wananchi wa vijiji hivyo kuwa kampuni hiyo
ya uwindaji katika muda wote huo, haijafanya chochote kwa ajili ya
wananchi na kuikatisha tamaa wakati inatoa mamilioni ya dola, lakini
hawataki kusema ukweli wa mgawo huo.
“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa sisi hatuna ugomvi na jamii na tunaishi nao
vizuri sana na tunatoa misaada kwa hisani bila ya kusukumwa kila mwaka,
lakini msaada huo unaonekana kama si lolote,” alisema Mollel na
kuongeza: “Angalia kwa mwaka tunatoa kiasi hicho cha fedha cha dola za
Marekani 1,037,000 na pia halmashauri na hupewa tena asilimia 25 ya
mapato kutoka serikali kuu kwa kile tulicholipa kule hivyo kwa mwaka
halmashauri hiyo hupata zaidi ya shilingi bilioni nne.”
Akizungumzia changamoto zinazowakabili katika hicho kilichohudhuriwa
pia na Mkurugenzi wa Wanyamapori nchini, Profesa Alexander Songoro,
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (Tawiri), Dk Simon
Mduma, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Allan
Kijazi na Ofisa Misitu Mkuu, Nurdin Chauya, mkurugenzi huyo wa OBC
alisema ni kuwa na wawekezaji wawili ndani ya pori hilo kinyume cha
mkataba.
Wengine waliohudhuria kikao hicho ni pamona na Mkurugenzi wa Mamlaka
ya Usimamizi wa Wanyama Pori Nchini (TAWA), Martin Loiboki, Naibu Waziri
wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, ambaye ni mbunge wa Ngorongoro, William Ole
Naasha, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Lekule Laizer, Mkurugenzi wa
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Dk Fred Manongi.
Mollel alisema kwa mujibu wa mkataba walionao, pori hilo halipaswi
kuwa na wawekezaji wawili, lakini kwa sasa wana mwekezaji mwingine
Kampuni ya And Beyond iliyoingia mkataba na Kijiji cha Ololosokwan
kufanya shughuli za utalii wa picha na inalipa mamilioni ya fedha moja
kwa moja kijijini, tofauti na wao wanaolipa halmashauri.
Alisema pamoja na mkanganyiko huo, kuripotiwa sehemu husika yaani
serikalini, lakini wao wamekuwa wakiendelea kufanya kazi kwa ushirikiano
kwa kupeana zamu za kuwinda na kupiga picha ili kusiweze kuleta madhara
pindi wanapokutana mbugani.
Changamoto nyingine zinazowakabili ni pamoja na kuingiza mifugo kwa
wingi kutoka nchini na nchi jirani ya Kenya na kuharibu kwa kiasi
kikubwa uoto wa asili na kuharibu vyanzo vyote vya maji kwa asilimia
kubwa na kufanya wanyama kuhama katika pori hilo.
Mollel alisema OBC inapendekeza kuwa taratibu na sheria za
wanyamapori zinapaswa kufuatwa na kusimamiwa kikamilifu, ikiwemo
matumizi bora ya ardhi, kuzuia mifugo kuingia katika pori hilo, kulinda
kwa vyanzo vya maji kwa gharama yoyote na kutokomeza kilimo ambacho
kinakuwa kwa kasi katika pori hilo bila ya sababu za msingi.
Diwani wa Kata ya Ololoswokani, Yannick Ndoinyo ambaye aliwakilisha
mapendekezo ya jamii inayozunguka pori hilo, alisema mgogoro wa pori la
Loliondo ulikua zaidi pale Waziri wa Maliasili na Utalii wakati huo, Dk
Khamis Kagasheki alipotangaza kuwa kilometa za mraba 1,500 kuwa ni pori
tengefu.
Ndoiyo alisema jamii inaona kuwa ufugaji na uhifadhi vinawiana
pamoja, hivyo hawaoni kama kuna tatizo na kusema kuwa ikifanyika hivyo
mgogoro huo utakuwa historia na malisho na kilimo kitambulike kisheria
katika pori hilo tengefu la Loliondo.
Mtafiti Mkuu wa Taasisi ya Wanyamapori, Edward Koho alisema vyanzo
vya maji vilikuwa vikipeleka maji katika Hifadhi ya Serengeti ambavyo
viko katika Pori la Tengefu la Loliondo vimekufa kutokana na uharibifu
wa mifugo na kilimo kikubwa kinachofanyika katika pori hilo kinyume cha
sheria za uhifadhi.
Baada ya kusikiliza mapendekezo ya awali ya jamii, wawekezaji na
wataalamu, Gambo alisema yatawakilishwa katika kamati na kufanyiwa kazi
kabla ya kupelekwa kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kama alivyoagiza ili
kumaliza mgogoro huo uliodumu kwa zaidi ya miaka 25.
chanzo;habarileo.
Comments