Kamati yaipa maagizo serikali wadaiwa sugu wa maji.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Dk Mary Nagu KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji imeitaka Wizara ya Maji na Umwagiliaji kupeleka orodha ya wadaiwa sugu wa maji nchini ili waijadili, waombe idhini ya Spika wa Bunge ili wawafikishe kwa Waziri Mkuu wachukuliwe hatua.
Uamuzi wa kuomba orodha hiyo ya wadaiwa sugu wa maji ilikuja baada ya kamati hiyo kujadili orodha ya waidawa sugu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (Duwasa) ambayo inazidai taasisi za serikali takribani Sh bilioni 1.9.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk Mary Nagu alisema anaitaka orodha hiyo ikabidhiwe kwenye kamati hiyo Ijumaa ijayo ili waijadili na kuomba idhini ya Spika wa Bunge ili wamfikishie Waziri Mkuu ili kuona namna ya kuzichukulia hatua.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge alisema madeni hayo yamekuwa sugu kutokana na ukweli kwamba yamekuwa yakikwamisha mamlaka za maji nchini kufanya kazi zake za uboreshaji wa huduma za maji nchini.
Lwenge alisema hadi sasa taasisi za serikali nchini zinadaiwa na Mamlaka za Maji nchini, zaidi ya Sh bilioni 34 fedha ambazo zinakwamisha mamlaka hizo kutekeleza majukumu yake.
Emmanuel Papian (Kiteto-CCM) alisema wakati umefika kwao kama kuonesha uwajibikaji wa kamati katika kuisaidia wizara ili kuzisaidia mamlaka za maji kulipwa fedha hizo kwa ajili ya kuendeshea shughuli mbalimbali ikiwamo ya kuboresha miundombinu.
Papian alisema wizara inatakiwa kuandaa orodha na wao wataomba idhini kutoka kwa Spika wa Bunge ili kufikisha wadaiwa hao kwa Waziri Mkuu.
DUWASA inazidai taasisi mbalimbali za serikali takribani Sh bilioni 1.9 likiwamo Jeshi la Polisi Sh 615,847,654, Magereza Sh 262, 771, 479, Hospitali ya Mkoa wa Dodoma Sh 168, 216,686 na JWTZ Sh 110,484,514, JKT Makutopora Sh 512,188,442, Hospitali ya Mirembe Sh 193,086,157 na Ofisi ya Makamu wa Rais Sh 60,131,633, Ofisi ya Waziri Mkuu Sh 17,123, 672, Sekondari ya Dodoma Sh 8,710,852 na Sekondari ya Msalato Sh 8,055,901.
Makamu wa Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk Christina Ishengoma alisema ni muhimu orodha hiyo kuletwa mbele ya kamati ili itoe msukumo wa namna ya kusaidia mamlaka za maji zilipwe ili kuboresha miundombinu.
chanzo;habarileo.

Comments