Hospitali Dar zahitaji madaktari wa mifupa.

Moja ya majengo ya Taasisi ya Tiba na Mifupa Muhimbili (MOI).MKOA wa Dar es Salaam umesema kuwa huduma ya tiba ya mifupa inafanyika katika hospitali zake za rufaa ambazo ni Temeke, Amana na Mwananyamala.

Pale tatizo linapokuwa kubwa, mgonjwa hupelekwa katika Taasisi ya Tiba na Mifupa Muhimbili (MOI).

Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk. Daisy Majamba alisema jana alipokuwa akizungumza na Habari Leo kuhusu mikakati ya mkoa katika kuisaidia MOI hususani kwenye suala la majeruhi wa ajali.

Dk. Majamba alisema kwa hospitali hizo, ilitakiwa kuwepo angalau madaktari bingwa wa mifupa 12, kwa maana kuwa kila hospitali ilipaswa kuwa na madaktari wanne.

Lakini, alisema kwa sasa hospitali ya Amana ina daktari moja, Temeke daktari mmoja na Mwananyamala hawana daktari bingwa.

Alisema wagonjwa wengi wanapopata ajali, huanza kupelekwa katika hospitali hizo, lakini inapoonekana ana shida kubwa anahamishiwa MOI. Kwa upande mwingine, MOI imetoa takwimu za majeruhi kwa miaka saba iliyopita kuanzia mwaka 2010 hadi mwaka jana, ambazo zimeonyesha majeruhi wa bodaboda, magari, bajaji, baiskeli na watembea kwa miguu.

Taarifa kutoka Kitengo cha Takwimu MOI, inaeleza kuwa takwimu za majeruhi wa bodaboda kwa miaka hiyo saba ni 14,285. Majeruhi wa magari kwa miaka hiyo saba ni 13,861 , bajaji ni 421, baiskeli 547 na kwa ajali zile zisizojulikana vyanzo vyake majeruhi walikuwa 31614.

Takwimu zinaonyesha kuwa kwa mwaka jana pekee 2016 majeruhi wa bodaboda walikuwa 3273, na wa magari walikuwa 1385, bajaji walikuwa 45 na baiskeli 102.

Jana Mkurugenzi wa Tiba wa MOI, Dk. Samuel Swai aliishauri Serikali kuongeza uwezo katika hospitali zake za mkoa jijini Dar es Salaam, ama kujenga taasisi nyingine kama hiyo nne.

Hatua ambayo itapunguza msongamano wa majeruhi wa ajali wanaotibiwa hapo, ambao wastani kwa siku ni wagonjwa 30.

Pia aliishauri Serikali kuijengea taasisi hiyo utaalam wa kuelimisha wataalam zaidi katika kuhudumia majeruhi wa ubongo, uti wa mgongo, mishipa ya fahamu na viungo vikubwa kama nyonga na magoti.

chanzo;habarileo.

Comments