Dk. Shein: Mjenga nchi ni mwananchi.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa licha ya kuwepo kwa mabadiliko ya mifumo ya uchumi katika karne hii ya ishirini na moja, bado ukweli unabakia kwamba mjenga nchi ni mwananchi hivyo jamii iache dhana kwamba watu kutoka nje ndio watakuja kuijenga Zanzibar.

Dk. Shein aliyasema hayo leo katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la Hoteli ya Verde-Mtoni Marine, iliyopo Mtoni nje kidogo ya mji wa Zanzibar inayomilikiwa na “Bakhresa Group of Companies”.

Dk. Shein alisema kuwa  ni lazima wananchi washirikiane, waipende nchi yao na kufanya kazi kwa bidii kwani kila mmoja ana nafasi akiwa Zanzibar au nje ya Zanzibar ya kutoa mchango wake adhimu kwa ajili ya kuijenga Zanzibar

Dk. Shein alitoa pongezi kwa Mwenyekiti wa “Bakhresa Group of Companies”, Said Salim Bakhresa kwa umahiri, ari na ujasiri wake wa kuyatekeleza kwa vitendo mambo anayoyaahidi, anayoyasema na anayoyaamini sambamba na uzalendo alionao katika kushirikiana na Serikali pamoja na wananchi katika kuijenga Zanzibar.

Hata hivyo Dk. Shein alieleza kuwa Serikali itaenda sambamba na watendaji waliokuwa hawaiwezi kasi ya maendeleo iliyokusudiwa na kusisitiza kuwa watendaji wazembe hawatovumiliwa hasa wale wanaodhorotesha masuala ya uwekezaji.

Alieleza kuwa wawekezaji wanataka watu wakweli na hawataki wababaishaji hivyo aliwasisitiza watendaji wote kufanya kazi zao kwa ufanisi huku akisisitiza kuwa watakaoshidnwa kwenda na kasi hiyo watakaa pembeni.

Pia, Dk. Shein alieleza faraja yake kutokana na hoteli hiyo kuja kutoa ajira zaidi ya 1200 ambalo hilo ni jambo muhimu katika kipindi hichi ambacho suala la ajira ni changamoto kwa vijana wa hapa nchini.

Alieleza juhudi zinazochukuliwa na Serikali katika kujitangaza kiutalii, na jinsi idadi ya watalii inavyoongezeka sambamba na juhudi zinazofanywa kati ya Serikali na mashirika ya ndege mbali mbali duniani ili yafanye safari za kuja Zanzibar ambapo hivi karibuni Shirika la Uturuki limeanza safari za kuja Zanzibar rasmi.

Dk. Shein alieleza umhimu wa kuwepo wka mashirikiano kati ya Serikali na Sekta binafsi katika kukuza na kuutangaza utalii huku akisisitiza suala zima la amani na utulivu nchini kwa faida ya kila mmoja na kuwasihi wananchi kuimarisha amani na utulivu ili utalii uendelee kukua hapa nchini.

Pia, alieleza haja ya kujidhatiti katika kuuimarisha utalii wa ndani hapa Zanzibar kwani kuna vitu vingi ambavyo nchi nyengine havipo na kutumia fursa hiyo kueleza kuwa ujenzi wa hoteli hiyo unatarajiwa kukamilika mwezi wa sita mwaka huu.

Nae Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Khalid Salum Mohammed alipongeza hatua za makusudi zinazofanywa na Kampuni hiyo ya Bakhresa kwa kushirikiana na Serikali katika kuimarisha sekta ya utalii ambayo ndio inayoongoza katika kukusanya mapato.

Alieleza kuwa wananchi wanafarajika kwa kiasi kikubwa na juhudi za Dk. Shein za kuleta maendeleo na kusema kuwa kukamilika kwa hoteli hiyo kutachangia uchumi wa nchi sambamba na kutoa huduma kwa jamii ikiwemo suala zima la ajira na kuahidi kuwa  Wizara yake itaendeleza ushirikiano na Kampuni hiyo katika miradi yake yote.

Nae Mkurugenzi wa Mamlaka ya Uwekezaji wa Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA), Salum Khamis Nassor alieleza majukumu na shughuli za Mamlaka hiyo na jinsi ilivyoshirikiana na Kampuni ya Bakhresa Group katika kuanzisha mradi huo pamoja na na fedha zaidi ya Dola milioni 20 zitakazotumika hadi kukamilika kwake.

Mapema Mwakilishi wa Kampuni ya Bakhresa Group of Companies Salim Aziz alieleza kuwa ujenzi wa hoteli hiyo ya kisasa ya kitalii ya hadhi ya nyota tatno ambayo ni rafiki wa Mazingira unaendelea na itakuwa na vyumba 106 vikiwemo 6 vyenye hadhi ya kutumiwa na Marais.

Aidha, alisema kuwa hoteli hiyo itakuwa  ni ya kisasa kabisa na ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na kupata usajili wa kuwa na uhifadhi mkubwa wa Mazingira kwani itakuwa inatumia umeme wa jua, mitambo maalum ya kurejesha maji yanayotumika hotelini na makasha maalum ya kutenganisha aina za taka.

Hoteli hiyo itakuwa na ukumbi wa mikutano, michezo ya maji, eneo maalum kwa ajili ya kuegesha boti za kitalii ambapo pia kutakuwa na boti ndogo ndogo kwa ajili ya kwuapelekea watalii katika visiwa vya Prison Islan na vyenginevyo pamoja na mambo mengineyom hoteli hiyo pia itakuwa na uwezo wa kutumiwa na watu zaidi ya 2500.

Hafla hiyo ya uwekaji wa jiwe la msingi la hoteli hiyo ni miongoni mwa shamra shamra za maadhinisho ya miaka 53 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya Januari 12, 1964 ambayo ilipambwa na ngoma za utamaduni, taarab asili na utenzi.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

chanzo;zanzibar24.

Comments