Hivyo, Dk. Shein aliwasisitiza wananchi kuzingatia hekima ya wazee
kwamba kinga ni bora kuliko tiba na badala yake ni vyema kila mmoja
akajiwekea muda maalum wa kufanya mazoezi yanayolingana na afya na umri
wake.
Dk. Shein aliyasema hayo leo mara baada ya kushiriki kikamilifu
katika maadhimisho ya Siku ya Mazoezi Kitaifa huko katika uwanja wa
Amaan, Mjini Zanzibar yalioanza uwanja wa Tumbaku hadi uwanja wa Amaan
mapema saa 12 za asubuhi,
Viongozi mbali mbali walishiriki mazoezi hayo akiwemo Rais mstaafu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi, Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, viongozi wengine wa dini na
serikali pamoja na vikundi vya mzoezi kutoka Unguja, Pemba na Tanzania
Bara.
Katika hotuba yake Dk. Shein alisema kuwa mazoezi ni lazima hasa
katika dahari hizi ambapo mfumo wa maisha umekuwa na changamoto nyingi
zitokanazo na kuongezeka kwa mahitaji na hamkani za maisha ya kisasa
hapa nchini na duniani kote.
Alisema kuwa hivi sasa jamii imeacha utamaduni wa kutembea kwa miguu
na kwa baskeli badala yake hupanda vyombo vya moto hata kwa masafa
mafupi huku akieleza athari za vyakula vya kisasa vikiwemo mahanjumati,
michuzi ya mafuta, mapochopocho yalionona ambayo hupikwa kwa samli za
kisasa na kuacha vyakula vya asili.
Dk. Shein aliwahakikishia wananchi kwamba Serikali itaendelea na
juhudi za kuimarisha michezo na kuviunga mkono vikundi mbali mbali vya
mazoezi ya viungo ikiwa ni pamoja na kuweka miundombinu bora ya michezo.
Alisema kuwa Serikali imedhamiria kujenga viwanja vya michezo katika
kila wilaya Unguja na Pemba ambapo tayari imeanza mchakato kwa viwanja
vitatu kikiwemo kiwanja cha Kitogani Mkoa wa Kusini Unguja, Mkoa wa
Kaskazini Unguja na Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Dk. Shein aliwaahidi wana mazoezi na wana michezo wote kwamba
Serikali italifanyia kazi ombi lao la kuwapatia mafunzo walimu wa vilabu
vya mazoezi ili waendeshe michezo na mazoezi kwa njia na mbinu za
kitaalamu zaidi.
Aidha Dk. Shein alilitaja jambo linalodhorotesha juhudi za kuimarisha
michezo kuwa ni uchache wa wadhamini katika ngazi zote za michezo
ambapo kampuni nyingi zilizopo Zanzibar na Wafanyabiashara bado hawana
mwamko wa kutosha wa kutumia michezo kwa kujitangaza.
Hivyo Dk. Shein aliutaka uongozi wa Wizara ya Habari, Utalii,
Utamaduni na Michezo kwa kushirikiana na Baraza la Michezo la Zanzibar
pamoja na vyama vya michezo kubuni mikakati mipya kwa kuzishawishi
Kampuni na Wafanyabiashara kutumia michezo kujitangaza.
Dk. Shein alisisitiza michezo kuzingatia nidhamu na kuwataka
wanamichezo wasisahau kuwa dhamira ya michezo ni kuburudisha na
kuunganisha na sio kugombanisha.
Kwa upande wa kombe la Mapinduzi , ambapo mara hii michuano maalum ya
vijana katika Wilaya zote za Unguja na Pemba imeanzishwa na kusisitiza
kuwa timu za Zanzibar lazima zifanye vizuri ili kombe la Mapinduzi mara
hii libaki hapa hapa Zanzibar.
Dk. Shein alitoa shukurani kwa uongozi wa Wizara ya Habari,
Utamaduni, Utalii na Michezo na uongozi wa Chama cha Mchezo wa Mazoezi
ya Viungo (ZABESA) kwa maandalizi mazuri ya Bonanza hilo na hatimae
kutoa vyeti maalum kwa wale wote waliofanikisha Bonanza hilo.
Nae Waziri wa Habarim Utalii, Utamaduni na Michezo, Rashid … aliahidi
kuwa Wizara yake itaendelea kushirikiana na vikundi vya michezo na
mazoezi huku akitumia fursa hiyo kumpngeza Dk. Shein kwa kuanzisha siku
maalum ya mazoezi Kitaifa.
Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar, Sharifa Khamis
alimpongeza Dk. Shein kwa kuwathamini na kuwajali wanamichezo wa
Zanzibar na kueleza jinsi wanavyofarajika na juhudi zake katika kuinua
sekta ya michezo hapa nchini.
Mapema katika risala yao wafanyamazoezi ya viungo walieleza kwamba
kutofanya mazoezi kunaongeza hatari ya kupatwa kwa ugonjwa wa moyo na
kuzisha hatari ya shinikizo kubwa la damu na pia huongeza maradufu
uwezekano wa kufa kwa shinikizo la damu na kiharusi.
Walieleza kuwa mwamko wa kufanya mazoezi nchini umeongezeka huku
wakieleza umuhimu wa mazoezi kwa watoto na hatimae kueleza changamoto
yao ya kuhitaji kupatiwa walimu wa vilabu mafunzo ya kufanya mazoezi
kitaalamu zaidi kwa maslahi ya Taifa.
Bi Rukia Ramadhani nae hakua nyuma katika kutoa burudani ambayo
ilitumbuiza hadhara iliyokuwepo kwa nyimbo yake maalum ya kumpongeza Dk.
Shein ambaye ni muasisi wa Bonanza hilo ambapo pia wanamazoezi hao nao
walipata fursa ya kuonesha mazoezi mepesi pamoja na vikundi vya
sarakasi navyo vilionesha umahiri wao.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
chanzo; zanzibar24.
Comments