Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed
Shein aliyasema hayo katika hafla ya uzinduzi wa vifaa vipya vya
kufanyia kazi bandarini, hafla iliyofanyika katika Bandari ya Malindi
mjini Unguja ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za miaka 53 ya Mapinduzi
ya matukufu ya Zanzibar.
Aliwataka wafanyakazi Bandarini hapo kuwa waaminifu na waadilifu
zaidi, kuepuka urasimu katika kutoa huduma, kujiepusha na vitendo vya
rushwa na zaidi kuhakikisha kuwa wateja wanahudumiwa kwa muda mchache
bila ya kukiuka taratibu ziliopo.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alikemea tabia ya baadhi ya wafanyakazi
wa Bandari kufanya kazi kinyume na maadili na taratibu za kazi zao na
kueleza kuwa endapo wakijulikana wale wote wanaofanya kazi hivyo
watashughulikiwa ikiwa ni pamoja na kushtakiwa ama kufukuzwa kabisa
kazi.
Pia, Dk. Shein alieleza jinsi ya mapato yanavyopotea katika Bandari
hiyo ya Zanzibar kutokana na wafanyakazi wachache wasiotimiza wajibu wao
ipasavyo ambao hufanya hila na udanganyifu ikiwa ni pamoja na kupitisha
vitu vilivyopitwa na muda wa matumizi vikiwemo vyakula.
Kutokana na hilo, Dk. Shein ametoa wiki moja mambo hayo yasitokee
tena, ikiwa ni pamoja na kukomesha hila zinazofanywa bandarini hapo na
baadhi ya wahusika za kutoa makontena bure na kupelekea kuikosesha
Serikali mapato.
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa hatua ya ununuzi wa vifaa hivyo ni
mafanikio ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi wa CCM ya mwaka 2015 hadi
2020 ambayo imeanza kutekelezwa kwa kasi ikiwa ni pamoja na kuiendeleza
Bandari ya Malindi kwa kuipatia vifaa na kukamilisha ujenzi wa bandari
mpya ya kuhudumia mizigo katika eneo la Mpigaduri.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alisema kuwa Serikali itaiimarisha na
kuiendeleza Bandari ya Mkoani kwa kuipatia vifaa vya kisasa vya
kuhudumia abiria na mizigo ambapo pia, Serikali inaendeleza mazungumzo
na wawekezaji kwa lengo la kuiimarisha Bandari ya Wete kutokana na
umuhimu wake kwa Serikali, wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Pemba na
watumiaji wote.
Kwa upande wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Dk. Shein alisema kuwa
Serikali itaendelea kuiimarisha gati ya Mkokotoni kwa kukamilisha ujenzi
wa jeti kwa ajili ya huduma za usafiri wa wananchi hasa wa Mkokotoni na
Tumbatu.
Dk. Shein alisisitiza haja kwa uongozi wa Wizara ya Ujenzi,
Mawasiliano na Usafirishaji pamoja na Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika
hilo kuwaangalia wafanyakazi wanaoendesha vifaa hivyo kiafya na
kimaslahi na kutoa pongezi zake kwa ununuzi wa vifaa hivyo.
Nae Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafiorishajim Ali Abeid Karume
alisema kuwa mafanikio hayo yametokana na uongozi bora wa Dk. Shein
ambapo licha ya azma ya Serikali kujenga Bandari mpya huko Mpigaduri
lakini alisisitiza haja ya kununuliwa vifaa hivyo muhimu bandarini hapo.
Mapema Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mustafa Aboud Jumbe alisema kuwa
jumla ya TZS Bilioni 11.8 zimetumika katika kununua vifaa hivyo vikiwemo
Kreni 2, Terminal Tractor 2, Terminal Trailer 2, Reach Stacker 3, Empty
Container Hanler 1, Forklift 3 na maboya ya solar 7.
Alisema kuwa vifaa hivyo vinatoka nchini Sweden, Belgium, Italy na
Ujerumani ambapo vimeingia nchini kati ya Mei hadi Disemba, 2016 na
tayari vimeanza kutumika kwa majaribio ambapo alisisitiza kuwa kuwasili
kwa vifaa hivyo kutasaidia sana kuongeza uwezo wa Bandari kuhudumia
mizigo pamoja na kuongeza kasi ya ushushaji na upakiaji wa mizigo.
Viongozi mbali mbali walihudhuria katika hafla hiyo akiwemo Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Spika wa Baraza la
Wawakilishi Zubeir Ali Maulid na viongozi wengine wa Serikali vyama vya
siasa na dini.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk.
chanzo: zanzibar24.
Comments