Akizungumza na waandishi wahabari jana, Ofisa Msimamizi wa chama
hicho anayesimamia Mkoa wa Dar es Salaam, Mark Serra alisema Chakua
imekuwa ikifuatilia kwa karibu mfumo huu na kubaini una manufaa makubwa
kwa abiria, ambapo watatozwa nauli halali iliyoidhinishwa na Sumatra,
ambazo ndizo bei elekezi kwa mujibu wa sheria.
Alisema kwa kutumia tiketi za kielekroniki, itawalazimu wamiliki wa
vyombo vya usafiri kutokupandisha nauli katika kipindi cha mvua au jua
kali, kipindi cha wanafunzi wapotoka vyuoni au mashuleni pamoja na
kipindi cha sikukuu au mwanzoni mwa mwaka, ambapo mabasi mengi huita
vipindi hivyo ni vya kuvuna abiria.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa chama hicho, Hassan Mchanjama alisema
kutumika kwa mfumo huo, utawanufaisha abiria na kuokoa muda wa kwenda
kwenye vituo vya mabasi kwa ajili ya kukata tiketi badala yake mfumo huu
utamuwezesha abiria kukata tiketi akiwa nyumbani, ofisini au sehemu
yoyote kwa kutumia simu yake ya mkononi.
Alisema mfumo huo pia utarahisisha upatikanaji wa taarifa muhimu za
abiria pindi inapotokea ajali kujua abiria wangapi wamepoteza maisha,
waliopata ulemavu pamoja na waliopoteza mali zao, ambapo kwa mfumo
unaotumika sasa hivi ni vigumu kupata takwimu na taarifa sahihi za
abiria.
“Naamini kupitia mfumo huo wa kielekroniki Chakua itakuwa katika
nafasi nzuri zaidi ya kutekeleza jukumu lake la kumtetea abiria pindi
anapopata tatizo kwa kuwa itakuwa na taarifa sahihi za abiria, na hakuna
abiria atakayepata shida wakati wa kusafiri,” alisema.
chanzo;habarileo.
Comments