Katika ufuatiliaji huo, jana bodi hiyo ilikwenda katika kampuni tatu,
Kampuni ya ndege ya Precision, Kampuni ya Mantrac na kampuni ya
vinywaji baridi ya Pepsi (SBC Tanzania Limited ).
Wakiwa katika ofisi za Precision, walishindwa kuonana na uongozi
baada ya katibu muhtasi kukataa kutoa ushirikiano kwa madai hawakuwa na
miadi na uongozi wa kampuni hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya tukio hilo, Mkurugenzi
Msaidizi wa Urejeshaji Mikopo wa HELSB, Phidelis Joseph alisema,
amesikitishwa na kitendo kilichofanywa na Precision.
Alisema licha ya kampuni hiyo kugoma kutoa ushirikiano, lakini
wamekuwa na tabia ya kulimbikiza marejesho, jambo ambalo sio sahihi na
kupeleka baadhi ya majina huku mengine wakiyaacha.
“Leo (jana) tumekosa ushirikiano wamegoma kuonana na sisi, kampuni
hii ni moja ya ambazo zimekuwa na usumbufu na kushindwa kuleta marejesho
kwa wakati wanapaswa kulipa Sh milioni saba kwa mwezi wameshindwa
kufanya hivyo na kusababisha kuwa na deni la Sh milioni 31 kama faini
kwa kuchelewa kupeleka marejesho kwa kipindi cha miezi 20,” alisema.
Aidha alisema idadi iliyotolewa na kampuni hiyo ni ndogo
ukilinganisha na idadi ya watumishi katika kampuni hiyo ambayo vyanzo
vya bodi hiyo imebaini uwepo wa wanufaika wengine katika kampuni hiyo
lakini majina yao hayajapelekwa na mwajiri katika bodi hiyo.
“Haiwezekani kampuni kama Precision iwe na wanufaika saba tu shirika
zima, sisi tunatambua wapo zaidi ya hao saba tunachokitaka walete majina
ya wanufaika wote na pia walete marejesho kwa wakati ili fedha hizo
zitumike kwa wanafunzi wengine wanaohitaji kupata mkopo na kama
wakishindwa kufanya hivyo watachukuliwa hatua za kisheria,”aliongeza.
Akiwa Pepsi, Joseph alisema, kampuni hiyo imekuwa ikisumbua kwa muda
mrefu, kwani wametengeneza bili ya watu zaidi 45 waliorodheshwa kama
wanufaika tangu Septemba mwaka 2015, lakini hawajapeleka fedha na kila
mara wamekuwa wakiwasiliana na kiongozi wa kampuni hiyo, lakini amekuwa
akionesha dharau bila kutoa ushirikiano, jambo ambalo ni kinyume cha
sheria.
“Tunashangaa hapa makao makuu hawaleti fedha hizo lakini katika
matawi yao ya Moshi na Arusha wamekuwa wakilipa tunataka leo wamtume mtu
ofisini kwetu kuchukua majina ambayo tumeyaorodhesha na majibu ya
kwanini wameshindwa kulipa kwa muda mrefu pamoja na majina halali ya
wanufaika na wakishindwa tutawachukulia hatua,”alisema.
Katika Kampuni ya Mantrac, Joseph alisema kampuni hiyo imeonekana
kuorodhesha majina machache, ili hali vyanzo vya bodi hiyo vinafahamu
uwepo wa wanufaika wengine wanaofanya kazi hapo.
Pia alisema kampuni hiyo imeshindwa kulipa marejesho tangu mwezi
Julai mwaka jana, hivyo amewataka kuhakikisha wanalipa malimbikizo hayo
kwa wakati ili kuepuka faini.
“Tumezungumza na Meneja rasilimali watu na tumemueleza ameahidi
kufuatilia na kuhakikisha wanaleta marejesho ambayo wameyalimbikiza kwa
wakati na kufuatilia kuona kama kuna wanufaika zaidi walioajiriwa lakini
majina hayajatufikia,”aliongeza.
Kwa upande wake, Mwanasheria wa bodi hiyo, Wambura Mkono alisema,
waajiri wanatakiwa kuwasilisha majina ya wafanyakazi wao ndani ya siku
28 baada ya kuwaajiri ili waweze kuwaangalia endapo ni wanufaika au la;
na atakapojulishwa kuwa ni wanufaika, anatakiwa kumkata asilimia 15 ya
mshahara wake na kuiwasilisha bodi ya mkopo kabla ya tarehe 15 ya mwezi
unaofuata katika kalenda.
chanzo;habarileo.
Comments