Bandari ya Mkoani Pemba sasa kutoa huduma za kimataifa.

Shirika la Bandari Zanzibar  limejipanga kuimarisha miundo mbinu yake katika kuona Bandari ya Mkoani Kisiwani Pemba inatoa huduma zinazokidhi kiwango cha Kimataifa.

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA ) tayari imeshatoa idhini na kutangaza kwamba Bandari ya Mkoani  Pemba inaweza kutoa huduma za Kimataifa ikiwemo shughuli za kupokea na kusafirisha Makontena kutokana na kukuwa kwa biashara katika Kisiwa hicho.
Msaidizi Mkurugenzi wa Shirika la Bandari Tawi la Pemba Nd. Hamad Salum alieleza hayo wakati Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar balozi Seif alipofanya ziara ya kukagua shughuli za Bandari hiyo akimalizia ziara yake ya siku Tatu Kisiwani Pemba.
Ndugu Hamad alisema Uongozi wa Shirika la Bandari tayari umeshaanza hatua ya kufanya maboresho ya maboya, Umeme pamoja na huduma za Maji safi na salama yanayokwenda sambamba na Ununuzi wa Krini ya Kuteremshia Vitu vizito Bandarini.

Alisema hatua hiyo imekuja baada ya kukamilika kwa Utafiti wa Kitaalamu wa kuiangalia upya Banadari hiyo uliofanywa mwaka 2016  kwa lengo la kuunga mkono maamuzi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania.
Msaidizi Mkurugenzi huyo wa Shirika la Bandari Tawi la Pemba alimueleza  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Bandari ya Mkoani hivi  sasa inaendelea kupokea Meli za mizigo na Abiria kutoka Unguja na  Mombasa Nchini Kenya.
Alisema kwa sasa Bandari hiyo imeshapokea meli zenye uwezo wa kubeba Tani 200 kutoka Unguja na Makontena 300 yenye ujazo wa Tani 300 kutoka Pemba licha ya kwamba bado wapo baadhi ya Wafanya biashara wenye kigugumizi cha kuteremsha makontena yao moja kwa moja kutoka nje ya Zanzibar.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar Nd. Abdulla Juma alisema kwa Vile Shirika lake tayari limeshanunua Krini Moja ya kuteremshia Mizigo, uwezo wa kushusha makontena ya wafanya biashara katika Bandari ya Mkoani upo na kinachohitajika kwa sasa ni Wafanya biashara hao kuyaamini mazingira hayo.
Ndugu Abdulla alisema lengo lililowekwa na Uongozi wa Shirika lake ni kuona Mizigo ya Wafanya biashara kutoka Nje ya Zanzibar inakwenda Pemba moja kwa moja badala ya kupitia kisiwani Unguja na Mombasa Nchini
Kenya.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema wazo la Uongozi wa Shirika hilo la Bandari kuimarisha Bandari ya Mkoani ni jema na la msingi kwa sababu litasaidia kufungua njia zaidi za Kibiashara kati ya Visiwa vya Zanzibar na Mataifa mengine Duniani.
Balozi Seif alisema shughuli za Bandari ni miongoni mwa maeneo ambayo Serikali Kuu inategemea kuongeza Mapato yake sambamba na kupanuka kwa fursa za ajira zitakazowanufaisha Wananchi Wazalendo hasa Vijana.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuagiza Uongozi wa Shirika la Bandari na washirika wake vikiwemo vyombo vya Ulinzi kuhakikisha kwamba udhibiti wa uingiaji na utokaji katika maeneo ya Bandari unaimarishwa ipasavyo.
Alisema wapo baadhi ya watu hutumia harakati za wasafiri kuingiza mambo yao ikiwemo usafirishaji wa bidhaa haramu lakini pia uingiaji wa wageni wasiozingatia sheria na utaratibu uliowekwa na Taifa wa Uhamiaji.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alitembelea Hospitali ya Rufaa ya Abdulla Mzee iliyopo Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba  kuangalia huduma za Afya zinazotolewa na watendaji wa Hospitali hiyo.
Daktari Mkuu wa Hospitali ya Abdulla Mzee Dr. Haji Mwita Haji alimueleza Balozi Seif  kwamba mazingira bora ya miundombinu ya Vifaa, Majengo na watendaji yamepelekea Wananchi wa Kisiwa cha Pemba kuwa kimbilio la kutaka kupata huduma za Afya.
Hata hivyo Dr. Haji Mwita alisema zipo changamoto zinazoikabili Hospitali hiyo pamoja na Watendaji wake akazitaja baadhi kuwa ni pamoja na umbali wa Makaazi ya watendaji hao jambo ambalo linaleta
usumbufu wakati inapoteka uchelewaji wa usafiri.

Dr. Mwita alizitaja changamoto nyengine  kuwa ni uhaba wa Dawa, huduma za umeme wa dharura, ongezeko la wagonjwa pamoja na utaalamu mdogo wa watendaji wake kwa baadhi ya amashine za Kisasa zilizomo ndani ya Hospitali hiyo na kushairi kuandaliwa mpango maalum wa kupatiwa mafunzo.
Akizungumza na baadhi ya Madaktari na watendaji wa Hospitali hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Madaktari na Wauguzi wa Hospitali hiyo wanalazimika kuwajibika ipasavyo ili hadhi ya Hospitali hiyo iendelee kubakia.
Balozi Seif  alisema mfumo huo wa uwajibikaji ulioambatana na vifaa vipya na vya kisasa unaweza kushawishi wagonjwa kutoka nje ya Visiwa vya Zanzibar kutaka kupatiwa huduma za Afya kwenye Hospitali hiyo ya Abdulla Mzee Mkoani.
Alielezea masikitiko yake kutokana na Hospitali nyingi nchini kulalamikiwa kutokana na huduma zake hawa wakiguswa zaidi Wauguzi kutokana na kauli zao za kuwavunja moyo wagonjwa wanaokwenda kutaka kupatiwa huduma za Afya.

Akizungumzia Makaazi ya Madaktari wa Hospitali hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari imeshaamua kujenga nyumba Nne za Ghorofa kwa nia ya kuondosha tatizo
hilo.
Alisema Serikali kupitia Wizara ya Afya imeshazungumza na Kampuni iliyojenga Hospitali hiyo kwa ajili ya kuangalia uwezekano wa kujenga Nyumba hizo ili kupunguza gharama za kumtafuta mkandarasi mwengine wa
ujenzi huo wakati utakapowadia.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar katika nasaha zake kwa watendaji hao wa Hospitali ya Rufaa ya Abdulla Mzee Mkoani Pemba alisema Serikali isingependa kuona huduma za afya zinazotolewa kwenye Hositali hiyo zinaambatana na ushabiki wa Kisiasa.
Balozi Seif alisema Hospitali ni sehemu ya huduma inayompasa mwananchiye yote mwenye matatizo ya kiafya anapatiwa huduma zinazostahiki bila ya ubaguzi wala itikadi za kisiasa.
Alionya kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haitamvumilia mtendaji ye yote wa Sekta ya Afya atakayeonekana ana tabia hiyo yakushabikia masuala ya Kisiasa.


Comments