Alisema mpango huo wa Kitaalamu utaweza kutoa muelekeo wa kina kwa
kuzitambua nyumba zote zilizochakaa na ambazo kwa mazingira ya Mji huo
haziwezi tena kuhudumia makaazi ya Wananchi wake.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa agizo hilo mapema asubuhi alipofanya
ziara fupi ya kulikagua Jengo la Ghorofa Tatu la Kamisheni ya Wakfu na
Mali ya Amana katika Mtaa wa Hurumzi ndani ya Mji Mkongwe wa Zanzibar
baada ya kuporomoka wakati mafundi wakiwa katika harakati za
kulifanyia matengenezo makubwa.
Maporomoko hayo yaliyomfunika Fundi Mmoja aliyetambuliwa kwa jina la
Khamis Kombo yalisababisha kifo chake kilichothibitishwa na Kamanda wa
Polisi Mkoa Mjini Magharibi na Fundi mwengine kulazwa Hospitali Kuu ya
Mnazi Mmoja baada ya kujeruhiwa vibaya.
Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kamwe
haitovumilia kuona Wananchi wake wanaendelea kuishi katika mazingira
hatarishi ndani ya nyumba ambazo itathibitishwa na Uongozi na Wataalamu
hao wa Mamlaka ya Mji Mkongwe kwamba hazistahiki kuishi Wanaadamu.
Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uhifadhi na Utunzaji wa Mji
Mkongwe wa Zanzibar Nd. Issa Sarboko Makarani alisema Uongozi wa
Mamlaka hiyo pamoja na ule wa Shirika la Nyumba Zanzibar uko katika
hatua ya mwisho ya kufanya mazungumzo ili Wataalamu wake wafanye zoezi
maalum la kuzikagua nyumba zote za Serikali zilizomo ndani ya Mji huo.
Nd. Sarboko alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba
zoezi hilo litabainisha wazi Ngumba zilizoharibika kabisa na kuwa
katika mazingira hatarishi jambo ambalo juhudi za makusudi
zitachukuliwa katika kuona lile fungu dogo la fedha linalopatikana
lielekezwe katika kuziokoa kwanza nyumba hizo.
“ Tunatarajia kuwa na zoezi la pamoja kati yetu sisi watu wa mamlaka
ya Mji Mkongwe na wenzetu wa Shirika la Nyumba Zanzibar kuzikaguwa ili
tuzitambue nyumba za Serikali zilizo katika hali mbaya na baadaye
kuzifanyia matengenezo ya dharura ”. Alisema Nd. Issa Sarboko Makarani.
Naye kwa upande wake Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Ayoub Mohamed
Mahmoud alisema Uongozi wa Serikali ya Mkoa wake hautokubali kuridhia
malalamiko yanayotolewa na yatakayoendelea kutolewa na baadhi ya watu
dhidi ya Serikali kwa uamuzi wake wa kuhami maisha ya wananchi wake.
Mheshimiwa Ayoub alisema jambo la msingi litakaloendelea kuchukuliwa
na kutiliwa mkazo na Serikali ni dhima ya kuhami uhai wa maisha ya Raia
wakati panapojitokeza dalili za maafa bila ya kujali kasumba za kisiasa
zinazopigiwa debe na baadhi ya watu wakiwepo pia wanasiasa.
Ujenzi wa jengo hilo la Ghorofa Tatu Mali ya Kamisheni ya Wakfu na
Mali ya Amana Zanzibar ulikuwa unafanyika kwa mujibu wa sheria na
taratibu zote za mamlaka ya Uhifadhi na Utunzaji wa Mji ya mkongwe wa
Zanzibar.
Kikosi cha zimamoto na Uokozi Zanzibar kilifika katika eneo la tukio
mara baada ya kuanguka kwa ukuta wa mbele wa Nyumba hiyo na kujaribu
kumuokoa fundi aliyefukiwa na kifusi ambae tayari alikuwa ameshafariki
Dunia na maiti yake kupelekwa hospitali kuu ya Mnazimoja kwa uchunguzi
kabla ya kukabidhiwa familia kwa ajili ya mazishi.
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
chanzo:zanzibar24.
Comments