Alisema mafanikio ya mradi huo tayari yameanza kuonekana katika
ujenzi wa michirizi ya maji ya mvua kwenye maeneo ya Daraja Bovu, Mnazi
Mmoja, Kijangwani na baadhi ya maeneo ya Jang’ombe na Wananchi wake
tayari wanafaidika na matunda ya mradi huo.
Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati wa hafla ya Uwekaji wa Jiwe
la Msingi la Ujenzi wa Ukuta wa Ukingo wa Bahari hapo Mizingani
Forodhani Mjini Zanzibar ikiwa ni miongoni mwa harakati za shamra shamra
za kusherehekea miaka 53 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Alisema Serikali ya Mapinduzi imejipanga kuimarisha miradi hiyo
ikiwa sehemu ya Jududi za utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya
Mwaka 2015 ikilenga kuwaondoshea usumbufu unaowakumbwa wananchi walio
wengi hasa wale wa maeneo ya Ng’ambo ya Mji.
Balozi Seif alisema ujenzi wa Ukuta wa Ukingo wa Bahari hapo
Mizingani Forodhani Mjini Zanzibar ukiwa miongoni mwa miradi ya Jamii
Mijini ni muhimu kwa maendeleo ya Mji Mkongwe wa Zanzibar uliobahatika
kuwemo kwenye Miji ya urithi wa Dunia ambao unategemewa kwa uchumi wa
Taifa kwa upande wa Sekta ya Utalii.
Alifahamisha kwamba Ukuta huo pamoja na bara bara yake, njia ya
waendao kwa miguu, na ujenzi wa Bustani ya Forodhani utabadilisha
mazingira na mandhari ya eneo zima la Mizingani, Forodhani pamoja na Mji
Mkongwe kwa ujumla utachochea kuimarika kwa shughuli mbali mbali za
Kijamii na Kitalii.
Balozi Seif aliwaomba Wananchi katika maeneo mbali mbali nchini
kuendelea kuwa na sura katika kipindi hichi cha mpito katika uimarishaji
na ujenzi wa miundombinu hiyo iliyoelekezwa katika miradi yao ya
Kijamii.
Hata hivyo Balozi Seif aliwanasihi Wananchi kufanya juhudi ya
kuitunza miradi hiyo wakati itakapokamilika ujenzi wake kwa kuacha tabia
ya kutupa taka taka kwenye michirizi iliyojengwa ili iweze kupitisha
maji machafu vizuri.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amempongeza mshirika mkubwa wa
Maendeleo wa Zanzibar, Benki ya Dunia {World Bank } kwa misaada yake
kadhaa inayotoa kwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika Sekta za
Elimu, Miundombinu pamoja na huduma za Kijamii akiitolea mfano Sekta ya
Afya.
Balozi Seif aliwahakikishia Wananchi kwamba kupitia mradi huo wa
Jamii Mijini Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakusudia kuendelea na
awamu ya pili ya uwekaji wa Taa za Bara barani kutoka Mwanakwerekwe
hadi Kiemba samaki, Uwanja wa Ndege hadi Mnazi Mmoja na Mikunguni hadi
Muembenjugu kwa upande wa Unguja.
Alisema kwa upande wa Kisiwa cha Pemba Serikali itaweka Taa za Bara
barani katika Miji yote Mitatu ya Pemba , Wete, Chake chake na Mkoani
kupitia mradi wa huduma za Jamii Mijini {ZUSP}.
Aidha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisisitiza kwamba kupitia
Mradi huo kutoka Mkunazini hadi eneo lote la Majengo ya Nyumba za
Maendeleo Michenzani litaboreshwa kwa kazi itakayokwenda sambamba na
ujenzi wa Jaa la Kisasa katika mtaa wa Kibele Wilaya ya Magharibi :B”
litakalohudumia Mji wa Zanzibar.
Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar Nd. Khamis Mussa Omar alisema chimbuko la mradi
wa ujenzi wa ukuta wa Mizingani umetokana na athari kubwa iliyojitokeza
siku za nyuma ya kasi kubwa ya maji ya Bahari iliyoathiri eneo hilo.
Alisema Ujenzi wa Ukuta huo ulioanza Tarehe 22 April 2015 ukiwa na
urefu wa Mita 320, upana Mita sita na ongezeko na mita sita kuelekea
usawa wa Bahari unatarajiwa kukamilika rasmi ndani ya Mwaka huu wa 2017.
Alieleza kwamba asilimia 65% ya ujenzi huo imekamilika kwa upande wa
ukuta wenyewe na kazi iliyobaki na kuendelezwa kwa hivi sasa ni ujenzi
wa bustani pamoja na bara bara ya watembeao kwa miguu.
Nd. Khamis alisema Mradi wa Jamii Mijini unaotekelezwa na Serikali
kupitia Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar chini ya mkopo nafuu kutoka
Benki ya Dunia umejigawa sehemu tatu katika utekelezaji wake akizitaja
kuwa ni pamoja na kuimarisha Taasisi, Mabaraza ya Miji pamoja na
usimamizi wa mradi husika.
Akimkaribisha Balozi Seif kuzindua ujenzi huo wa Ukuta, Waziri wa
Fedha na Mipango Dr. Khalid Salum Mohamed alisema uimarishaji wa Mji
Mkongwe kupitia mradi wa Jamii Mijini utakuwa chachu ya kuimarika kwa
Sekta ya Utalii Nchini.
Dr. Khalid aliwaomba Wamiliki Binafsi wa majengo yaliyomo ndani ya
Mji Mkongwe kushirikiana na Serikali Kuu katika kuyaweka kwenye
mazingira bora yatakayotoa haiba nzuri ya Mji wa Zanzibar unaotegemewa
katika makusanyo ya Mapato ya Taifa kupitia sekta hiyo ya Utalii.
Ujenzi wa Ukuta wa Ukingo wa Bahari hapo Mizingani Forodhani Mjini
Zanzibar unasimamiwa na Wizara ya Fedha na Mipango ya Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Mkono wenye masharti nafuu wa shilingi
Bilioni 7,222,577,890 kutoka Benki ya Dunia.
chanzo:zanzibar24.
Comments