Alisema hatua hiyo muhimu itawapa hamasa zaidi Wakulima wa zao hilo
kuongeza juhudi za uzalishaji kupitia Mradi wa kuongeza Tija na
uzalishaji wa Mpunga Zanzibar { ERPP } unaoonekana kuleta mafanikio
makubwa ya kipato tokea kuanzishwa kwake katika kipidi kifupi
kilichopita.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa agizo hilo wakati akizindua rasmi uvunaji
wa Mpunga wa Umwagiliaji maji kwa kutumia Teknolojia ya Shadidi
inayosimamiwa na Benki ya Dunia hapo katika bonde la Mpunga Cheju Wilaya
ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.
Alisema Zanzibar inaweza kupunguza uagizaji wa bidhaa za vyakula kama
mchele kutoka nje ya nchi kutoka asilimia 80% hadi 40% ifikapo mwaka
2020 iwapo mkazo utaongezwa na wananchi walio wengi Vijijini
wanaojihusisha na Kilimo katika kutekeleza mradi huo.
Alieleza kwamba Kilimo cha mradi wa shadidi ndio mkombozi
pekeeunaoweza kuipunguzia Serikali kutumia fedha nyingi za Kigeni kwa
ajili ya kutumiwa na wafanyabiashara kuagiza bidhaa hiyo nje ya Nchi.
“ Lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kupunguza uagizaji wa
bidhaa za vyakula kutoka nje ya nchi kwa kuongeza uzalishaji mara dufu
“. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwashukuru washirika wa
Maendeleo wa Kimataifa kwa jitihada zao za kuendelea kuiunga Mkono
Zanzibar katika kuimarisha Miradi ya Maendeleo.
Alisema Zanzibar bado inaendelea kuungwa Mkono na Washirika mbali
mbali wa Maendeleo Duniani na kuiomba Wizara ya Kilimo, Maliasili,
Mifugo na Uvuvi kuendelea kutafuta washirika wengine wa Maendeleo
watakaoweza kusaidia mipango ya Taasisi hiyo ili kuwaongezea nguvu zaidi
za uzalsiahji wakulima wa Visiwa hivi.
Akisoma Risala kwa niaba ya wakulima wa Mradi wa Kilimo cha Mpunga
wa umwagiliaji Maji kwa kutumia Teknolojia ya Shadidi Mmoja wa
Wakulima hao alisema mradi huo umeleta mafanikio makubwa yaliyopelekea
Robo eka kuvuna kati ya Polo 13 na 14 ikilinganishwa na kilimo cha
zamani walichoambulia Polo 8 hadi 9.
Alisema pamoja na mfanikio hayo alizitaja changamoto zilizojitokeza
katika harakati zao za kilimo ikiwa ni pamoja na ukosefu wa usawa wa
ardhi katika mabonde ya Kilimo hicho unaosababisha baadhi ya ploti
kukosa maji ya uhakika ya kuimarisha kilimo hicho.
Wameiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iongeze wawekezaji zaidi
watakaoshirikiana nao katika kuimarisha miundombinu itakayosaidia
kufanikisha Mradi huo wa Kuongeza Tija na uzalishaji katika zao la
Kilimo.
Mapema Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Mh. Hamad Rashid
Mohamed alisema Teknolojia hiyo ya Shadidi ndio pekee inayoweza
kuwakomboa Wakulima wakizingatia kufundishana kwa hatua ya awali ya
kuona.
Mh. Hamad Rashid alisema Hekta 500 pekee ndio zenye miundombinu ya
Kilimo cha Umwagiliaji Maji kati ya Hekta 8,500 za Mabonde yote ya
yaliyomo Visiwani Zanzibar.
Alisema ushirikiano wa pamoja kati ya Viongozi, Wataalamu wa
Kilimo, Wananchi na wakulima wenyewe katika kuyatumia vyema mabonde
yaliyobakia ya kilimo kwa kuendeleza Mradi wa Shadidi unaweza kupunguza
au kuondosha kabisa uagizaji wa mchele kutoka nje ya Zanzibar.
chanzo:zanzibar24.
Comments