Baba, mwanawe wauawa kwa ujambazi.

WANAKIJIJI wa Ncheli Kata ya Sungwizi Tarafa ya Simbo wilayani Igunga mkoani Tabora wameua majambazi watatu kati ya watano wakiwemo baba na mwanawe baada ya kumvamia Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ncheli, kumjeruhi kisha kumpora pikipiki na fedha.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Hamisi Selemani alithibitisha kuuawa kwa majambazi hao watatu ambao wawili wametambulika kuwa ni Nkuba Mwadi (55) na Bundala Nkuba (35) wakazi wa kijiji hicho cha Ncheli huku jambazi wa tatu anayekadiriwa kuwa na miaka 25, hakutambulika jina lake wala makazi yake.
Aidha, Kamanda Selemani alisema pikipiki waliyoiba kwa mwalimu ipo katika Kituo cha Polisi Igunga.
Hakuna mtu anayeshikiliwa na polisi hadi sasa.
Diwani wa Viti Maalumu Kata ya Sungwizi, Anjel Milei amesema, majambazi hao walivamia nyumbani kwa Mwalimu Joseph Samweli saa 5:00 usiku wa kuamkia juzi ambako walivunja mlango kwa kutumia jiwe kubwa maarufu fatuma.
Milei alifafanua kuwa baada ya majambazi hao kuvunja mlango, waliingia ndani ya nyumba hiyo na kuanza kumshambulia mwalimu kwa mapanga na kumpiga kwa nondo hadi kumvunja mkono wa kushoto na kusababisha kupoteza fahamu.
Alisema baada ya majambazi hao kuona mwalimu ameanguka chini, walimwamuru mkewe awapatie funguo ya pikipiki na kadi yake, na mama huyo alitekeleza amri hiyo. Hata hivyo, pamoja na mama huyo kutoa vitu hivyo majambazi hao hawakuridhika na ndipo yalimwamuru atoe fedha, hali iliyomfanya atoe Sh 150,000.
Aidha, diwani huyo alidai baada ya majambazi hao kuona wamepata vitu hivyo waliamua kuondoka na vitu ikiwemo pikipiki, televisheni na vitu vingine ambavyo thamani yake inafika Sh milioni 3.6.
Baada ya wanakijiji kuona majambazi wameondoka ndipo walijikusanya na kuanza kuwafuatilia huku wengine wakimkimbiza mwalimu katika Hospitali ya Rufaa Nkinga ambako amelazwa akiendelea kupatiwa matibabu.
Diwani Milei alifafanua kuwa wanakijiji hao walipofika katika Kijiji cha Kaumbu kilichopo Kata ya Nanga walimpata jambazi mmoja akiwa na pikipiki na televisheni na wakati akihojiwa na wanakijiji hao ili awataje wenzake alianza kuwashambulia kwa nondo baadhi ya wanakijiji hali iliyowachukiza na kumtembezea kipigo hadi kufa papo hapo.
Aidha wananchi hao waliamua kuwasaka majambazi wengine aliokwishawataja majina yao kabla mauti haijamfika.
Hata hivyo, waliwapata majambazi wawili baba na mwanawe nao waliwatembezea kipigo hadi kufa.


Mwalimu aliyejeruhiwa Samwel (44) akizungumza wodini hospitalini Nkinga, alisema hakutegemea kama atazungumza kwa kile alichosema walimjeruhi vibaya kwani mkono wake ulivunjika na kuomba serikali iwatengenezee mazingira mazuri walimu juu ya usalama wao wanakoishi ili wafundishe kwa amani.
chanzo;habarileo.

Comments