Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi, Ado Shaibu, alisema chama hicho leo kitawasilisha malalamiko hayo na kwamba kinalaani vitendo vinavyofanywa na watendaji wa serikali hasa katika kata ya Nkome.
"Katika kata ya Nkome iliyoko wilayani Geita, Halmashauri inavunja taratibu kwa kuanzisha kazi ya kuwakusanya wazee kwa lengo la kuwapatia huduma za matibabu bure wakiwataka waende na vitambulisho vya kupigia kura," alisema.
Shaibu alisema kwa kufanya hivyo watendaji hao wa serikali wanavunja sheria na taratibu za uchaguzi.
Mwaka jana Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema serikali itahakiki wazee nchi nzima ili wapatiwe vitambulisho maalumu vya kupata matibabu bure na kuanzisha dirisha maalumu katika hospitali nchini kwa ajili ya makundi maalumu, wakiwemo wazee.
"Na wale ambao walienda bila vitambulisho vya kupigia kura waliwekwa kando, maswali ya kujiuliza ni kwanini zoezi hili wakati wa kipindi cha uchaguzi, na ni kwa nini wazee hawa wanatakiwa kwenda na vitambulisho vya kupigia kura? Jibu ni dhahiri kuna lengo la kuwafanya wazee hao kukipigia kura CCM," alisema Shaibu.
Shaibu alisema kwa mujibu wa kanuni za maadili ya uchaguzi ambazo vyama vyote vinazifahamu ni marufuku watendaji wa serikali kutoa ahadi katika kipindi cha kampeni mpaka kipindi cha uchaguzi.
Alisema kanuni hizo ambazo CCM inazivunja ziliwekwa kwa lengo la kuweka usawa kwa vyama vyote vinavyoshiriki uchaguzi. Aidha, Shaibu alisema Chama cha ACT Wazalendo kimesimamisha madiwani katika kata tano Tanzania Bara na pia mgombea ubunge Dimani, Zanzibar katika uchaguzi utakaofanyika Januari 22, mwaka huu.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mkurugenzi wa wilaya ya Geita, Ally Kidwaka alisema wakati uchaguzi unaendelea na maisha nayo lazima yaendelee.
"Wenzetu nao lazima waelewe, wakati wa uchaguzi na maisha nayo lazima yaendelee, sisi tulikua na ratiba yetu ya kuandikisha toka 28 Novemba mwaka jana kwa Nkome ilikua jana (juzi) ni siku moja kila kata sasa hatuwezi kusimamisha kazi," alisema mkurugenzi huyo.
Alisema kama kuna chama ambacho hakiridhishwi na jambo lolote kuna kamati za maadili wapeleke malalamiko huko na sio kwenye vyombo vya habari na kwamba hali haiko hivyo kama inavyoelezwa.
chanzo;habarileo.
Comments