Waziri aoneshwa samaki wa mabomu.

SERIKALI imeshuhudia shehena ya samaki inayokaribia tani 1.3 wa thamani ya Sh milioni 13 katika soko la Kimataifa la Samaki, Feri jijini Dar es Salaam, waliovuliwa baharini kwa kutumia mabomu.
Shehena hiyo ya samaki wakiwemo aina ya kolekole, jodari, change, pono, sehewa na nguru iliingizwa sokoni hapo Ijumaa iliyopita na baada ya ukaguzi kufanywa katika zoni tatu na kubainika kuingizwa kwa samaki hao, huku wahusika wakitokomea.
Hata hivyo serikali imetoa siku saba kwa Bodi ya soko hilo kuhakikisha wahalifu hao wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria, pia ikiahidi kupeleka Bungeni sheria ya uvuvi wa bahari kuu ili ifanyiwe marekebisho na kitendo hicho kuwa ni cha uhujumu uchumi.
Akizungumza jana Dar es Salaam katika soko hilo, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba alikasirishwa na kitendo cha kutokamatwa kwa wahusika na kumtaka Mwenyekiti wa Bodi ya soko hilo, kupitia upya mfumo wa mapokezi, ulinzi na usimamizi katika soko hilo ili kujiridhisha kama uko safi.
“Mwenyekiti wa Bodi, ninachokutaka pitia upya mfumo wa mapokezi ya samaki, ulinzi na usimamizi wa ndani, mjiridhishe kama wako safi, la sivyo nitazungumza na Mamlaka ya Ilala ili muondoke wote na Wizara isimamie soko hili,” alisema Tizeba na kuongeza kuwa Tanzania imebaki peke yake inayotuhumiwa kwa kuvua kwa njia haramu.
Alisema ni aibu sana kwa kitendo hicho kufanyika tena ikiwa ni mita chache kufika Ikulu hivyo kama suala la ukaguzi limewashinda Bodi ya Soko waache kwa Mamlaka nyingine.
“Inasikitisha eti wote 13 waliohusika wameteleza, wametelezaje, kuanzia mwenye box (boksi) la kuwekea samaki, aliyefungua geti wakachambua na kuzihifadhi wamefanikiwaje,” alihoji Tizeba.
Dk Tizeba alisema waliohusika wakamatwe, polisi wapo, wafanye kazi hizo kwani wamejificha wasakwe, watangazwe kuwa ndio wanaoharamisha uvuvi, kwani wasipowatangaza watajua Serikali inawaonea aibu huku wakiendelea kulitia hasara taifa.
Alisema kitendo cha kuvua kwa mabomu sio kwamba kimeua samaki hao peke yake lakini wamekufa wengi zaidi na mazalia yameteketea, hapo walipokuwa hawawezi kuzaliwa tena.
Kuhusu sheria alisema yuko tayari kupeleka marekebisho ya sheria ya uvuvi wa bahari kuu Bungeni hata kwa hati ya dharura ili wahusika wa makosa ya aina hiyo wawe ni wahujumu uchumi na washindwe kulipa fidia kama ilivyo kwa sasa.
“Sheria imekaa vibaya, tutapeleka marekebisho bungeni hata kwa hati ya dharura kwani kwa sasa mhusika anapokamatwa na kosa la kuvua kwa mabomu, adhabu yake anaweza kulipa faini na kuondoka zake,” alisema Tizeba.
Alisema sheria hiyo ambayo ni mwaka 2003 na kanuni zake za mwaka 2009 lazima ifanyiwe marekebisho ili suala la kuvua kwa mfumo huo liachwe kuwa kosa la kihalifu peke yake bali liwe ni uhalifu wa uhujumu uchumi.
chanzo;habarileo.

Comments