Awali, mawakili upande wa watoa maombi wakiongozwa na Wakili Msomi, Juma Nassoro walitoa maombi ya kumtaka jaji ajiondoe kwa sababu ya hoja mbili ikiwemo ya wateja wake ambao ni Bodi ya Wadhamini CUF kutokuwa na imani naye.
Hata hivyo, Jaji Kihiyo jana amepingana na hoja za upande wa watoa maombi kwa kusema kuwa hoja zao hazikuwa za msingi.
“Nimezingatia hoja zilizotolewa na pande zote mbili za kuunga na kutounga mkono kujitoa kwangu zilizotolewa, pia nilipitia barua ya waombaji na kwamba madai ya waombaji hayana ukweli na hakukuwa na sababu za msingi zinazonishawishi kujitoa katika kesi,” amesema na kuongeza.
“Kwa mujibu wa sheria, jaji ana hiari ya kujitoa kama sababu au hoja zilizotolewa ni za msingi. Hivyo Ombi la kuniomba nijitoe halina mashiko na nalikataa.”
Aidha, Jaji Kihiyo amesema tarehe inayofuata ya kusikilizwa shauri hilo ambayo inatarajiwa kutajwa kesho, itatumika kusikiliza maombi ya mapingamizi ya pande zote mbili ambapo upande wa wadaiwa walipinga kusikilizwa shauri hilo jambo lililosababisha upande wa wadai pia kupinga maombi hayo.
Aidha, baada ya shauri hilo kusikilizwa Lipumba alidai kuwa kitendo cha Bodi ya Wadhamini kumtaka jaji kujiondoa kililenga kupoteza muda na kudai kuwa hawana hoja.
“Mawakili wao wameshindwa kusema ukweli, la kusikitisha wanatumia njia za kuzuia shauri hilo lisisikilizwe kwa haraka. Ninachokiona hapa kuna usanii wa kupoteza muda,” amesema.
Aidha, Bodi ya Wadhamini CUF ilifungua shauri hilo kwa hati ya dharura kwa madai ya kupinga hatua ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ya kumtambua Lipumba kama mwenyekiti halali wa CUF licha ya Baraza Kuu la Uongozi Taifa la chama hicho kumvua uanachama.
chanzo;zanzibar24.
Comments