MAOFISA wa Idara ya maendeleo ya Uvuvi Kisiwani Pemba, wanaiomba Serikali kupitia Wizara husika kuwapatia vitendea kazi vitakavyosaidia katika utafutaji na uwekaji wa taarifa za wafugaji wa Samaki pamoja na wakulima wa mwani.
Wameyasema hayo, baada ya kupatiwa mafunzo juu ya utafutaji na uingizaji wa taarifa kwa kutumia njia ya electronic kitaalamu (GPS) Geographical Position System katika program ya ( DATABASE).
Wamesema kuwa, mafunzo waliyopatiwa ni muhimu sana kwa kazi zao jambo ambalo litasaidia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa taarifa kwa wakati unapohitajika.
Sambamba na hayo, wamesema kuwa, Serikali kwa kuboresha utekelezaji wa shughuli za uvuvi kwa makusudi imeamua kutoa mafunzo hayo, ili taarifa ziweze kupatikana kwa usahihi na ubora kwa njia ya teknolojia.
Mmoja kati ya washiriki wa mafunzo hayo, Shaibu Masoud Said, ambae ni karani wa Diko la Msuka Pwani, amesema kuwa, mafunzo yamewapa muamko mkubwa juu ya utumiaji wa teknolojia na kwamba itasaidia kwa kiasi kikubwa katika kumbu kumbu za taarifa kwa wepesi zaidi.
Kwa upande wake, Ofisa wa mazao ya baharini Ali Khatib Ali, aliongeza kuwa, iwapo Serikali Itajipanga kuwatimizia vifaa, taarifa sahihi za takwimu kwa wakulima wa mwani na idadi ya mashamba itapatikana kwa matumizi ya Serikali na taifa kwa ujumla.
Nae, Mkufunzi wa mafunzo hayo, Hashim Hamza Chande, kutoka Wizara ya Kilimo, Maliasili Mifugo na Uvuvi Zanzibar, amewahimiza maofisa hao kuyazingatia vyema mafunzo hayo pamoja na kuyafanyia kazi inavyotakikana, ili kuisaidia serikali kupata taarifa za uhakika .
Akifunga mafunzo hayo, Ofisa mipango Idara ya Maendeleo ya Uvuvi, Ali Said Hamad, amesema kuwa, mafunzo yaliotolewa kwa hatua nyengine yatasaidia kuongeza utaalamu kwa watendaji hao, pamoja na upatikanaji wa taarifa mbali mbali za mambo ya bahari kwa muda mfupi.
Mafunzo hayo ya siku kumi (10) yaliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Kilimo ,Maliasili, Mifugo na Uvuvi Pemba, yaliwashirikisha Maofisa wa Idara ya maendeleo ya Uvuvi, Makarani wa madiko pamoja na maofisa wa mazao ya baharini.
Comments