Wamachinga watengewa maeneo.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally HapiMANISPAA ya wilaya ya Kinondoni, imetenga maeneo saba likiwemo viwanja vya Biafra vilivyopo Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT) kwa ajili ya wamachinga ambao hawana maeneo ya kufanyia biashara zao.

Akizungumza jana, Mkuu wa Wilaya hiyo, Ally Hapi alisema eneo hilo litakuwa likifanyiwa biashara siku ya Jumamosi na kwamba maeneo mengine yamepangiwa siku maalumu ambapo wamachinga watakuwa wanakwenda kufanya biashara.

Aliyataja maeneo mengine ni Kata ya Bunju katika Soko la Matunda ambako biashara zitafanywa siku ya Jumatano, Kijitonyama soko litaanzia kwenye mataa hadi stendi ya zamani siku ya Jumanne huku Kata ya Msasani, gulio litafanyika katika Soko la Magunia siku ya Jumapili.

“Katika Kata ya Mabwepande gulio litafanyika kwenye Soko la Bunju B siku ya Alhamisi, Kunduchi gulio litafanyika eneo la Meko siku ya Ijumaa na Kata ya Wazo gulio litafanyika eneo la Kisangu siku ya Jumatatu,” alisema Hapi.

Alisisitiza kuwa lengo la kugawa maeneo hayo ni kuwasaidia wafanyabiashara ndogondogo kwenda kufanya biashara katika maeneo yaliyopangwa kulingana na siku yake.

Aliongeza kuwa miundombinu mbalimbali katika maeneo yaliyotengwa yanaendelea kurekebishwa ikiwemo ujenzi wa vyoo vya kuhama.

Hapi alisema manispaa hiyo haina wafanyabiashara wengi isipokuwa maeneo ya Tegeta na Bunju ambako ndio kuna changamoto ya wafanyabiashara wadogo wadogo.

Pia alisema wafanyabiashara ambao hawatafuata agizo hilo watachukuliwa hatua za kisheria na kuwataka wazingatie usafi ili kuwa na maeneo bora zaidi.
chanzo;habarileo.

Comments