Hata hivyo, tume hiyo haikuweka wazi mali walizobaini kuporwa na
kueleza kuwa jambo hilo litafanywa na Mufti mwenyewe kwa kuwa ndiye
mwenye mamlaka ya kutoa taarifa za ripoti hiyo.
Akizungumza wakati wa kukabidhi ripoti hiyo katika Ofisi za Makao
Makuu ya baraza hilo, Kinondoni jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa
Tume hiyo, Shehe Abubakar khalid alisema tume hiyo imefanya kazi kubwa
hadi kukamilisha ripoti hiyo ya kwanza.
Shehe Hali alisema tume hiyo ilipewa miezi mitatu, lakini kazi hiyo
imekuwa ni ngumu hasa kwa kuzingatia kuwa baraza hilo lina mali nyingi
nchini kote na shughuli za tume hiyo ilikuwa ni kuhoji wahusika kwa
mikataba waliyoingia. “…Ilikuwa ni tabu kuwapata kwa nafasi zao ,
tumefanikiwa kukamilisha ripoti ya kwanza kwa baadhi ya mali tu na
mikataba ya mkoa wa Dar es Salaam, shughuli nyingine zitaendelea
baadaye,” alisema Shehe Khalid na kuongeza kuwa ripoti hiyo
waliyowasilisha ni nusu ya ripoti ya awali ya kazi ya Dar es Salaam na
wataendelea katika mikoa yote hadi watakapokamilisha na ndio sababu ya
kuomba waongezewe muda na wanamshukuru Mufti kwa kuwakubalia jambo hilo
kwa kuwaongeza miezi mitatu mingine.
Alisema walipewa hadidu za rejea zilizokuwa zikiwaeleza kufuatilia
viwanja, majengo pamoja na mali nyingine zilizokuwa zikimilikiwa na
Waislamu na ndilo walilolitekeleza. Naye Mjumbe wa tume hiyo, Shehe
Hamis Mataka alisema tume hiyo haina mamlaka ya kueleza kilichomo ndani
ya ripoti hiyo, bali mufti ndio mwenye mamlaka ya kueleza yaliyomo na
kuyafanyia kazi.
Alisema Mufti alitoa hadidu za rejea saba ambazo ni kufuatilia mali
za baraza hilo, kuangalia hesabu za baraza, kuangalia namna ya kuboresha
mifumo pamoja na mengine.
“Haya yote ndiyo yanayoshughulikiwa na tume, lakini kwa kuanzia
kutokana na ukubwa wa jambo, tume imeshughulikia yale yanayohusu Dar es
Salaam, sasa ukiulizia Dar es Salaam Bakwata ina viwanja vingapi? Ina
viwanja kadhaa, lakini kimojawapo ni Chang’ombe na mgogoro huo
unajulikana,” alieleza Mataka.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa ripoti hiyo, Mufti Zubeir alisema
kutokana na unyeti wa jambo hilo ameona awaongezee muda wa miezi mitatu
ili wamalize kazi hiyo nchi nzima.
“Nawashukuru tume kwa kazi ambayo nimewapa ambayo walikuwa waifanye
katika kipindi cha miezi mitatu na wakawa wamefanya kazi nzuri, lakini
kazi iliyofanywa ni nusu ya ile tunayotarajia tuipate na muda ukawa ni
mchache…nimeona niwaongezee muda wa miezi mitatu mingine kwa sababu
baraza lina mali nyingi nchi nzima,” alisema Mufti Zubeir.
Alisema ataisoma ripoti hiyo na baada ya hapo atafanyia kazi yote
yatakayokuwa yamebainishwa na kupendekezwa na ripoti ya tume hiyo. Mufti
kwa mamlaka aliyopewa na Katiba ya Bakwata, aliunda tume hiyo ambayo
ilianza kazi ya kufuatilia, kuhakiki na kuorodhesha mali za Waislamu
chini ya Bakwata Agosti 10, mwaka huu.
Katibu wake Salim Abeid, Wajumbe ni Omar Igge, Ali Ali, Taabu Kawambwa, Hamis Mataka na Mohamed Hamis.
Tume hiyo yenye wajumbe wanane iliundwa baada ya Rais John Magufuli
kuhutubia Baraza la Idd El Fitri, Julai 6, mwaka huu na kueleza
kusikitishwa na hatua ya baadhi ya watu wenye uwezo kutumia mwanya huo
kupora mali za Waislamu ambapo aliahidi kuzirejesha.
chanzo ;zanzibar24.
Comments