Hatua hiyo ya wanachama na viongozi hao imetokana na wao kubainika
ukiukwaji wa malengo ya kuasisiwa kwa umoja huo na badala yake ulitumiwa
na vyama shirikishi kukihujumu ambapo kuanzia uchaguzi wa Serikali za
Mitaa na ule Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka 2015.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mkutano wa ndani wa chama
hicho uliowashirikisha baadhi ya wanachama na viongozi wa kamati za
utendaji za wilaya za Kilosa, Mvomero, Morogoro Mjini na Vijijini
kichama, walimtaka Profesa Lipumba kuiondoa CUF ndani ya Ukawa kutokana
na madhara makubwa waliyoyapata.
Katibu wa Wazee wa CUF Wilaya ya Morogoro Mjini, Mohammed Chunga
alisema kutokana na kutokuwepo makubaliano ya kisheria ya kuachiana
majimbo na kata kutoka miongoni mwa washirika, kumekiathiri chama
kutokana na maeneo yaliyoachiwa CUF kuwekewa pia wagombea wa Chadema,
hatua hiyo ni pamoja na ngazi za udiwani.
Hivyo alisema sehemu ambapo mgombea wa CUF alikuwa akikubalika, pia
Chadema iliweka mgombea wake na kusababisha kura kugawanyika kitendo
kilichokinufaisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa mgombea wao kushinda kwa
tofauti chache za kura.
“Ukawa ndiyo chanzo kilichotuumiza sisi CUF bila kujitambua, hata
pale tulipokuwa tunakubalika na kuachiwa nafasi ya kusimamisha mgombea
ili tuungwe mkono na wenzetu washirika Chadema, NCCR Mageuzi pamoja na
NLD...tulijikuta tunawekewa mgombea wa Chadema...hili limetuumiza,”
alisema Chunga.
Na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya CUF Wilaya ya Morogoro
Mjini, Pilly Bilali, Awadhi Komba na Katibu mstaafu wa wilaya hiyo,
Haruna Msuku, kwa nyakati tofauti walisema hakuna mwanaCUF asiyetambua
Ukawa umewadhoofisha kisiasa upande wa Tanzania Bara na kikinufaisha
Chadema, hivyo kutaka ijiondoe mara moja.
Hata hivyo, wanachama na viongozi hao walimpongeza Profesa Lipumba
kwa uamuzi wake kurudi kwenye wadhifa wake na kwamba wataendelea
kumuunga mkono ili arudishe hadhi ya chama hicho baada ya kumalizika kwa
Uchaguzi Mkuu mwaka jana.
Akijibu hoja za wanachama na viongozi wa CUF wa wilaya hizo, Profesa
Lipumba alisema ushirikiano ndani ya Ukawa, vyama washirika viliwahujumu
katika uchaguzi uliopita. Profesa Lipumba alisema vyama washirika
walitumia mbinu mbalimbali ili kuwadhoofisha kwenye majimbo na kata
tofauti na makubaliano ya awali.
Hivyo alisema kutokana na wanachama na viongozi wa CUF sehemu
mbalimbali alizopita kukutana nao moja ya tatizo kubwa waliloliona ni
changamoto walizokutana nazo wagombea kwenye majimbo ya uchaguzi ulipita
na kwamba chama hakiwezi kurudia makosa hayo katika uchaguzi ujao.
Alisema Ukawa ilianzishwa na vyama vinne CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi
na NLD kwa lengo la kusimamia Rasimu ya Katiba ya Jaji mstaafu Joseph
Warioba na ili kuitetea, walianzisha Umoja wa Katiba ya Wananchi, hivyo
kuondoa tofauti zao za kivyama kwa msingi wa utetezi wa rasimu hiyo.
Hivyo alisema Ukawa si chama cha siasa na umekuwa kwa upande wa
Tanzania Bara na hautambuliki kwa mujibu wa sheria ya uanzishwaji wa
vyama vingi kwa maana hiyo kazi yake ni utetezi pekee wa rasimu ya
Katiba ya Jaji mstaafu Warioba na kwamba uhalali wake kwa sasa hauna
nguvu.
Alisema ushirikiano ndani ya vyama vya siasa upo kwa njia nyingi na
na iwapo utahitajika ni vyema ukajulikana kwa mujibu wa makubaliano ya
kisheria na si ilivyo sasa. Mbali na yaliyojitokeza siku za hivi
karibuni ndani ya CUF, Profesa Lipumba alitumia fursa hiyo kumtaka kila
mwanachama kushikamana na kuweka tofauti zao pembeni ili kukijenga upya
chama hicho.
chanzo;habarileo.
Comments